February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

KESI YA EPILEPSY ORGANIZATION DHIDI YA MWANASHERIA MKUU YAAHIRISHWA

Mahakama Kuu ya Tanzania masijala ya Dar es Salaam imeahirisha kesi iliyofunguliwa na Shirika liitwalo “Tanzania Epilepsy Organisation” dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali hadi tarehe 26 mwezi huu baada ya upande wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutokamilisha kujibu hati ya kiapo kinzani.

Shauri hilo linapinga Kifungu cha 39 (a)(ii) cha Sheria ya Ndoa kinachosema kwamba mume au mke anaweza kufungua shauri mahakamani ili ndoa yao ivunjwe kama wakati wanafunga ndoa mmoja kati yao alikuwa na kifafa.

Wakili wa serikali,Jacline Kinyasi ameiambia mahakama hii leo kuwa bado wapo ndani ya muda wa kisheria wa siku 14 wa kujibu hati ya kiapo kinzani na kuiomba mahakama ihairishe kesi hiyo ili kuwapa muda wa kuwasilisha maombi yao.

Kwa upande wake Wakili wa mleta maombi,Paul Kisabo alikubaliana na ombi hilo lililotolewa na upande wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Kesi hiyo inasikilizwa mbele ya jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu Jaji,S.Moshi,Jaji M.G.Mzuna na Jaji E.S Kisanya

Shauri hilo limeahirishwa hadi Aprili 26 mwaka huu saa 09:00asubuhi.