February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

KESI NDOGO YA MBOWE : USHAHIDI WAANZA KUSIKILIZWA

Mahakama ya Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumi uchumi imeanza kusikiliza ushahidi wa shauri dogo katika kesi ya uhujumu uchumi namba 16/2021 inayomkabili Freeman Mbowe na wengine watatu ambapo Upande wa Jamhuri umeieleza mahakama hiyo kuwa itatumia jumla ya mashahidi saba katika shauri hilo akiwemo Kamanda wa Polisi mkoa wa Kipolisi Kinondoni,ACP Ramadhani Kingai ambaye ameanza kutoa ushahidi wake hii leo.

Wakili wa serikali Mwandamizi Robert Kihando ameiambia mahakama hii leo wakati shauri hilo dogo lilipoanzwa kusikilizwa baada ya Jaji Mustapher Siyani kuridhia ombi la upande wa utetezi wa kufanya shauri hilo na kuwasilisha mapingamizi mawili dhidi ya  mshitakiwa Adam Hassan Kusekwa kuwa  aliteswa kabla na wakati wa kuchukuliwa maelezo .

Akitoa hoja za mapingamizi hayo Wakili Kibatala ameiambia mahakama kuwa maelezo ya Mtuhumiwa Adam Kasekwa yalichukuliwa nje ya muda kinyume cha Kifungu cha 50(1)(a)(b),(51na 52 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019 inayotaka maelezo yachukuliwe ndani ya saa nne tangu mtuhumiwa anapokamatwa.

Akiwasilisha ushahidi wake mahakamani hapo akiongozwa na Wakili wa serikali Robert Kihando  , ACP Ramadhani Kingai amekana mtuhumiwa Adam Kusekwa kuwa  aliteswa wakati akichukuliwa maelezo kwani hawakuwa na sababu za kufanya hivyo na kueleza kuwa mtuhumiwa alichukuliwa maelezo akiwa Central Police Dar es salaam akiwa na afya njema na baada ya kuandika maelezo hayo aliyasoma na kuthibitisha kilichoandikwa na Adam Kusekwa alikubaliana na maelezo hayo na kuweka saini kwa kutumia kalamu ya wino na dole gumba.

Aidha ameongeza kuwa zoezi la ukamataji halikuwa na shida yeyote tofauti na walivyodhani kwakuwa mtuhumiwa alikuwa komando na mtuhumiwa alitoa ushirikiano na hakukuwa na sababu za kutumia nguvu kumkamata. Pia ameeleza kabla ya kuanza kuchukua maelezo mtuhumiwa  alijulishwa haki zake ikiwemo alijitambulisha kwake na kama anaweza kutoa maelezo akiwa peke yake au apate ndugu,jamaa au wakili na mtuhumiwa alikubali kwa hiari kutoa maelezo akiwa peke yake.

Pia amesema mtuhumiwa Adam Kasekwa na Mohamed Lingwenya  walikamatwa tarehe 5/08/2020 katika eneo la Ruo madukani mijini Moshi  baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasiri wake kuwa walikuwa wakimtafuta  aliyekuwa Mkuu wa Wilaya wa Hai, Lengai Ole Sabaya ili waweze kumdhuru  na baada ya upekuzi walimkuta na kete 58 za madawa ya kulevya aina ya Heroin  na pistol moja ikiwa na risasi tatu , hatimaye walijaza hati ya upekuzi ambayo iliyosainiwa na mashahidi wawili aliowataja kwa jina la Anitha na Esta, watuhumiwa pamoja na wakamataji.

Akiendelea kutoa ushahidi wake ACP Kingai ameiambia mahakama kutokana na mazingira ya eneo la Ruo madukani kutokuwa rafiki waliamua kuwachukuwa mashahidi wawili hadi Central Police Moshi ili waweze kuchukuliwa maelezo kisha wakiwa na mtuhumiwa waliendelea kufanya ufuatiliaji wa Mtuhumiwa mwingine aitwaye  Moses Lijenge ambaye hadi tarehe 06/08/2020 hawakufanikiwa kumkamata na kuamua kurudi Dar es salaam ambako walifika alfajiri tarehe 07/08/2020 kwa hatua zingine zake.

Alisema kuanzia saa moja na nusu asubuhi hadi saa tatu kamili tarehe 7/08/2020 alianza kuchukua maelezo ya mtuhumiwa Adam Kasekwa kwa njia ya sauti  kwa kosa la kula njama za kutenda vitendo vya ugaidi, maelezo ambayo mtuhumiwa aliyathibitisha kuwa yalikuwa sahihi na kutia saini yake.

Wakati akihojiwa na Wakili wa utetezi Peter Kibatala shahidi ACP Kingai alieleza kuwa mtuhumiwa hakupewa onyo la kumiliki silaha kinyume na sheria na kukutwa na madawa ya kulevya na kosa ambalo walimkamata nalo mtuhumiwa ni kosa la kula njama za kufanya ugaidi na sio makosa mengine.

Baada ya kusikiliza ushahidi wake Jaji Mustapha Siyani ameahirisha kesi hiyo mpaka kesho tarehe 16/09/2021 majira ya saa nne asubuhi ambapo usikilizwaji wa shauri dogo utaendelea ili kumalizia ushahidi unaotolewa na shahidi wa kwanza wa upande wa Jamhuri ACP Robert Kingai.