February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

KESI NDOGO YA MBOWE: ACP KINGAI AENDELEA KUTOA USHAHIDI

Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu uchumi imeendelea kusikiliza ushahidi wa shauri dogo katika kesi ya Uhujumu Uchumi yenye mashitaka ya ugaidi inayomkabili Freeman Mbowe na wenzake watatu ambapo hii leo Shahidi namba moja wa upande wa Jamhuri, ACP Ramadhani Kingai ameendelea kutoa ushahidi wake katika shauri hilo.

Akiongozwa na Wakili mwandamizi wa serikali Robert Kidando ,ACP Kingai ameieleza mahakama kuwa hakutoa onyo la kumiliki silaha kinyume cha sheria kwa mshitakiwa Adam Hassan Kasekwa kwani aliamini kuwa tayari ameshamuonya kwa kesi kubwa ya kula njama za kufanya vitendo vya ugaidi na kwamba silaha inaweza kutumika katika kuteteleza vitendo hivyo.

Pia amesema mtuhumiwa  Adam Hassan Kasekwa alimueleza kuhusu ugonjwa wake wa Post traumatic stress disorder na kwamba hakufuatilia Zaidi kwani wakati akimuhoji  mtuhumiwa  alimueleza kuwa hana tatizo hilo kwa wakati huo  kwani alishapona baada ya kwenda kwao Mbeya ambako alipata matibabu na alirudi nyumbani kwake Chalinze kuendelea na kazi zake.

Aidha Kingai ameiambia mahakama kuwa hakuweza kuchukua maelezo ya mtuhumiwa Kituo Kikuu cha Polisi Moshi licha ya kuwepo kwa vifaa vyote muhimu kwasababu bado upelelezi mwingine ulikuwa ukiendelea uliofanya wasimhoji mtuhumiwa kituoni hapo na walikuwa wakimtumia mtuhumiwa pamoja na wasiri wake (Kingai) ili kufanikisha zoezi la kumkamata Moses Lingwenya.

Wakati akiendelea kuhojiwa na Wakili wa serikali Mwandamizi,Robert Kidando, Kingai ameieleza mahakama si lazima kuleta notebook kama kitendea kazi cha askari mahakamani, na kifaa hicho kinamwezesha askari kurekodi kuhusu kazi zake anazoweza kujikumbusha muda wowote na  kina vitu vingi na sio kitu kimoja tu.

Apoulizwa kuwa ni kwanini hakupeleka detention register ya polisi mahakamani, Kingai alieleza kuwa yeye sio msimamizi wa detention sheet hivyo kama itahitajika kutumika watu wanaohusika watakuja kutoa ushahidi

Baada ya kutoa ushahidi huo, Wakili wa serikali mwandamizi Robert Kidando aliiomba mahakama iahirishe shauri hilo hadi kesho ambapo wanakusidia kuleta mashahidi wengine wanaotoka nje ya mkoa wa Dar es salaam Kutoa ushahidi wao.

Jaji Mustapha Siyani baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili ameahirisha shauri hilo hadi kesho tarehe 17/09/2021 majira ya saa nne kamili asubuhi kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji wa shauri dogo upande wa mashahidi.

Usikilizwaji wa shauri hilo dogo ulianza saa sita nje ya muda uliopangwa kuanza kwa shauri hilo saa nne kamili asubuhi baada ya kuwepo kwa sintofahamu baina ya waliohudhuria kesi hiyo na maafisa wa polisi ambao waliwataka watu kutoingia na simu mahakamani hali iliyozua mjadala na kusababisha kesi kuchelewa kuanza kusikilizwa.

Hapo jana tarehe 15/08/2021 mawakili wa uteteziw aliweka mapingamizi mawili kuhusu mshitakiwa Adam Hassan Kasekwa kuwa aliteswa kabla na wakati akichukuliwa maelezo pia maelezo yake yalichukuliwa nje ya muda uliowekwa kisheria tangu akamatwe hivyo wakaiomba mahakama iendeshe shauri dogo.