February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

KENYA : MAHAKAMA YASEMA RAIS KENYATTA ALIKIUKA KATIBA KATIKA TEUZI ALIZOFANYA MWAKA 2018

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta

Mahakama Kuu nchini Kenya imeamuru kuwa uteuzi wa wakuu 128 wa mashirika ya umma uliofanywa na Rais Uhuru Kenyatta mwaka 2018 ni batili na haukuzingatia matakwa ya kikatiba.

Jopo la majaji watatu wa mahakama hiyo limesema uteuzi huo uliwajumuisha wanasiasa walioshindwa na kupoteza mwelekeo wa kisiasa na wakuu wa zamani wa serikali ulifanywa kinyume cha katiba na matakwa ya kisheria.

Katika uteuzi huo Rais Kenyatta aliteua watu maarufu akiwemo Mkuu wa Majeshi Mstaafu,Jenerali Julius Karangi,Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Walimu Kenya,Mudzo Nzili,aliyewahi kugombea kiti cha ugavana jimbo la Mombasa,Suleiman Shabbal na magavana wazamani Benjamin Cheboi,Doyo Godana na wengineo.

Katika uamuzi wake  mahakama imesema wakenya walitarajia uteuzi wa wakuu wa mashirika ya umma ungekuwa huru, wenye ushindani na wa uwazi na unapaswa ulipaswa kufanyika kwa kutangaza nafasi za ajira na wale waliotuma maombi kufanyiwa usaili ili kuwapa wananchi wote nafasi sawa suala ambalo halikufanyika.

Uamuzi wa Mahakama Kuu nchini humo umekuja baada ya Taasisi ya Katiba na Kituo cha Afrika cha Utawala bora nchini humo (AfriCOG) kuishitaki serikali kwa kutozingatia sheria wakati wa uteuzi wa wakuu hao.

Hii si mara ya kwanza kwa Mahakama nchini Kenya kutoa uamuzi mzito dhidi ya utendaji kazi wa Rais pale ambapo anakiuka sheria ambapo mnamo Mei 13 mwaka huu Mahakama Kuu iliamuru kuwa mchakato wa kubadili Katiba kupitia mpango wa BBI uliosimamiwa na Rais Kenyatta na kuungwa mkono na kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuwa ni kinyume cha sheria na kusema kuwa  Rais alifanya makosa ya kisheria alipokuwa akijaribu kubadili Katiba