February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

KAULI YA IGP SIRRO YA POLISI KUTOSOGELEWA NA RAIA YAKOSOLEWA

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umekosoa kauli aliyoitoa Mkuu wa Polisi nchini IGP Simon Sirro,Ijumaa, Agosti 27,katika viwanja vya Hospitali ya Polisi Kurasini,katika ibada ya kuaga miili ya askari Polisi watatu,na mlinzi wa kampuni binafsi ya ulinzi ya SGA,waliopoteza maisha kwa kupigwa risasi na mtu anayefahamika kwa jina la Hamza,eneo la Osysterbay,jirani na Ubalozi wa Ufaransa.

Katika salamu zake IGP Sirro,pamoja na mambo mengine alisema; “Walipomuona huyu mtu wa hovyo hovyo  Hamza anawasogelea,walijua ni mtanzania wa kawaida,kumbe alikuwa na bastola na akafanya alichofanya (Kuwaua askari kwa risasi),ni kitu tumejifunza,ukizubaa usilaumu jeshi,ukizubaa,usilaumu serikali.Askari mna Mafunzo ya kutosha,ni wakati sasa kwamba tuna changamoto kuwa siyo kila mtu ni rafiki”,mwisho wa nukuu.

Kauli hii imetafsiriwa kuwa inaweza kugeuka kuwa agizo,kwani kwa mujibu wa taratibu za majeshi yote,askari hufanya kazi kwa maagizo,na kwamba IGP Sirro hakutafsiri neno “rafiki” litumike kwa muktadha upi wa kipolisi,na kwa mtu gani polisi wawe nae makini akiwasogelea kwa sababu askari polisi wanaishi katika jamii na hawakwepi kuchangamana na jamii na kwamba tukio la askari kupigwa risasi na kuuawa lilikuwa tukio la kihalifu kama matukio mengine,na kwamba watanzania hawana utamaduni huo kwa kiwango hicho kama maelekezo ya IGP Sirro yalivyoelekeza.

“Tunakubaliana kabisa na IGP kwamba wakati wote askari wawe waangalifu,na wazingatie mafunzo yao waliyopewa wanapokuwa katika maeneo kazi yao,wakiwa na silaha,ni jambo ambalo tunakubaliana nalo kabisa.Lakini kauli yake kwenye hoja yake kuhusu umakini wa polisi wanaposogelewa,inaweza kutafsiriwa kwamba sasa hali ni tete,na kusema kuwa kila anayekuwa karibu na askari si rafiki,inaweza kuchukuliwa na askari kama kuweka mazingira magumu ya askari kuwa karibu na raia,na kitendo cha Hamza (Aliyewapiga polis risasi),siyo hali halisi ilivyo katika taifa,na inaweza kuleta taharuki kubwa na kufanya mazingira ya polisi kuwa karibu na raia kuwa magumu”,ameshauri Onesmo Olengurumwa,Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu,Tanzania.

Askari waliouawa kwa kupigwa risasi Agosti 25 jijini Dar es Salaam,waliagwa na kusafirishwa makwao kwa maziko,siku ya Ijumaa,katika zoezi lililoongozwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,George Simbachawene,viongozi mbalimbali wa serikali,pamoja na maafisa waandamizi wa polisi kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania.