February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

KATIBU MKUU TAMISEMI, SHEMDOE AWAJIA JUU WAKURUGENZI WANAOFICHA NYARAKA ZA WATUMISHI WANAOOMBA UHAMISHO

Na: Anthony Rwekaza

Kufuatia kuwepo madai kutoka kwa baadhi ya watumishi wa umma juu ya kucheleweshewa nyaraka za kuomba uhamisho,Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Prof. Riziki Shemdoe amekemea vikali na kuonya tabia hiyo kwa baadhi ya Wakurugenzi na watumishi wa Masjala wasio na weledi kuficha barua za uhamisho ambazo tayari zimesainiwa na Katibu Mkuu TAMISEMI,

Akizungumza na wananchi wakati akiwa kwenye ziara ya kikazi Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga iliyomalizika mwishoni mwa juma, Prof. Shemdoe amesema kuwa amekuwa akipokea malalamiko yasiyo isha juu ya mkwamo huo wa baadhi ya Barua za uhamisho kutokuwafikia watumishi waliopata uhamisho kwa kwa wakati.

“Kumeibuka wimbi la baadhi ya Wakurugenzi na Watumishi wa sehemu ya cha Masjala katika Ofisi za Mamlaka za Serikali za Mitaa kushindwa kutoa barua ambazo tayari zimesainiwa na Katibu Mkuu TAMISEMI na kutumwa kwenye Halmashauri, kwaajili yakuwapa wahusika lakini watu wachache kwa matakwa yao wamekuwa wakikwamisha Barua kwenda kwa wahusika, hili halikubaliki na hii ni kwenda kinyume na maadili ya Utumishi wa Umma.” ameonya Shemdoe.

Pia Prof. Shemdoe alisema, kufuatia malalaamiko hayo, hivi sasa Ofisi ya Rais TAMISEMI, inaendelea kufuatilia ili kubaini wale wote wenye kuendekeza vitendo hivyo, aidha kwa kiongozi yeyote wa Halmashauri au mtumishi atakayebainika kufanya unyanyasaji huo, basi sheria itachukua mkondo wake.

Aidha Prof. Shemdoe amedai vitendo ufanyika ili kutengeneza mazingira ya yenye viashiria vya rushwa ili waweze kukabidhi Barua hizo kwa wahusika, jambo ambalo amelikemea lisiendelee.

Kufatia changamoto hizo na nyingine zinazohusiana na uamisho wa watumishi wa umma waliochini ya TAMISEMI, Ofisi ya Rais TAMISEMI hivi sasa imeelekeza zoezi la uhamisho linafanyike kila baada ya miezi mitatu na barua zote za uhamisho zinasainiwa na Katibu Mkuu TAMISEMI, mara baada ya muombaji kukamilisha hatua zote muhimu ikiwa ni pamoja na barua hizo kupitishwa na mamlaka zao za ajira na kuombewa vibali kwa Makatibu Tawala wa Mkoa kabla yakuwasilishwa TAMISEMI kwa hatua za mwisho za uhamisho