March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

KATIBA MPYA YATAWALA BARAZA KUU CHADEMA

Kilio cha upatikanaji katiba mpya, kimetawala kikao cha Baraza Kuu la Chama cha Chadema, kilichofanyika Jumatano, tarehe 11 Mei 2022, kwenye ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

Viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa walioshiriki mkutano huo, wametumia fursa hiyo kuhimiza umarishwaji wa harakati za kudai katiba hiyo.

Zilizoshika kasi hivi karibuni baada ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuunda kikosi kazi maalumu cha kufanyia kazi maoni na mapendekezo ya wadau wa siasa juu ya maboresho ya demokrasia ya vyama vingi na mifumo ya utoaji haki nchini.

Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, amesema chama chake hakipingi ajenda ya upatikanaji tume huru , bali kinataka ajenda hiyo isiwe sababu ya kukwama kwa mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya.

“Ajenda ya tume huru ni ajenda yetu sote, lakini ajenda ya tume huru haipaswi kusimamisha mchakato wa katiba mpya, hata mambo yanapaswa kutegemeana,” amesema Mbowe.

Akizungumza katika kikaohicho, Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Babu Juma Duni Haji, amevitaka vyama vya siasa vya upinzani kusuka ajenda ya madai ya katiba mpya kwa wananchi badala ya kuishia ndani ya vyama hivyo.

“Katika ajenda yenu ya katiba mpya, tunahitaji mkitoka hapa tunakwenda kwa wananchi ili nyimbo iwe katiba mpya, katiba mpya ifike mpaka jikoni kule wanakopika kina mama, kila mtu atamke katiba mpya na umma uwe nyuma yetu,” amesema Babu Duni.

Aidha, Babu Duni amevitaka vyama vya siasa vishirikiane kwa pamoja katika kuleta mabadiliko ya uongozi nchini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Hashimu Rungwe, ameshauri vyama vya siasa viunge mkono msimamo wa chama chake katika kudai marekebisho makubwa ya katiba.

“Nyie wote mnajua CHAUMMA kilio chake ni katiba mpya, tunataka katiba mpya hakuna kingine, nafikiri wote tungesimamia hapo sababu hiyo mnasema sheria za uchaguzi zinazaliwa baada ya katiba kuwepo. Sheria za uchaguzi haziji bila katiba kuwepo,” amesema Rungwe na kuongeza:

“Kwa hiyo haya mambo kama hatuelewani wenyewe huku nje sisi sote kwa pamoja, hakuna maana. Wote tungeungana kuwa na katiba mpya ndiyo itatuondolea matatizo tuliyokuwa nayo halafu itafuata sheria za uchaguzi baada ya katiba kupatikana.”