February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

KALAMU YA WATETEZI:BARAKOA,LEVEL SEAT NA MSONGAMANO WA WATU VINAHITAJI NGUVU YA ZIADA TANZANIA.

Daladala ikiwa na abiria lukuki-Picha:Leonard Mapuli,Julai 26

Leonard Mapuli.

Jumapili Julai 25,Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ilitolea ufafanuzi wa  baadhi ya masuala muhimu yaliyoanishwa katika Mwongozo wa Udhibiti wa Ugonjwa wa Corona hapa nchini kupitia afua ya kudhibiti misongamano katika Jamii bila kuathiri shughuli za kiuchumi.

Kwa Mujibu wa kifungu A cha mwongozo wa  3.1.1, Imeainishwa kuwa, bodaboda wabebe kwa idadi sahihi (1-2) (siyo mishikaki) na wavae barakoa, Stendi zihakikishe zinatoa ujumbe wa kuelimisha jamii ya wasafiri mara kwa mara kupitia vipaza sauti, na wanapokuwa safarini, madereva na wahudumu wa vyombo vya usafiri wahakikishe ujumbe wa kuelimisha unatolewa kwenye chombo mara kwa mara, Wananchi wakae au kuongozana kwa umbali wa zaidi ya mita moja katika maeneo yote wanayokuwepo kabla ya kuingia kwenye chombo cha usafiri, Vyombo vya ulinzi na usalama vihakikishe magari ya usafiri wa umma wanapakia abiria kulingana na idadi ya viti pasipo kusimama; kwa magari maalumu yenye nafasi kubwa kama mwendokasi, inapolazimika kusimama basi kila abiria avae Barakoa na kuachiana angalau umbali wa nusu mita.

Katika mwongozo huu ndipo Gumzo likaibuka kila kona kujadili je!yanawezekanaje?

Watetezi Media imefika katika kituo cha mabasi cha Magufuli, Mbezi Louis mapema alfajili ya leo Julai 26,kabla ya mabasi ya kwenda mikoani kuanza kuruhusiwa kuondoka.Ni kweli kuwa karibu mabasi yote (Tuliyoshuhudia) yaliondoka na abiria wote waliokaa bila kusimama,huku mengine pia yakiwa na viti wazi.Idadi ya wasafiri wenye barakoa ilikuwa ni kubwa ikilinganishwa na wale wasiokua nazo,lakini msongamano ulikuwa ni mkubwa kama kawaida,tofauti na uwepo wa maji ya kunawa tiririka kwenye malango yote,bado msongamano ulikuwa hauna udhibibiti wala kujali kuhusu kujikinga kama ilivyoelekezwa na Wizara ya Afya.

Rais Samia Suluhu akiwa amevaa Barakoa.

Watetezi Media ilifanikiwa tena kufika katika vituo mbalimbali vya mabasi yaendayo kasikatika jiji la Dar es Salaan, kuanzia eneo la Mbezi hadi Kimara na kushuhudia mabasi yanayotoka kwenye maeneo hayo kuelekea mjini na kwingineko yakiwa na idadi kubwa ya watu waliosimama wengi,wengi wao hata bila barakoa wala kujali umbali kama ilivyoshauriwa na Wizara.

Vile vile katika vituo vidogo kuanzia Korogwe,Bucha,Baruti hadi Kibo, kumekuwepo na abiria wengine wengi waliosongamana katika kila kituo, kusubiri mabasi ambayo tayari yana abiria walioshonana kutoka Mbezi na Kimara kuelekea mjini,Morocco,na Muhimbili,huku pia abiria wakionekana kutojali suala la uvaaji barakoa na utakasaji mikono kwa namna yoyote.

Hali hii pia imeonekana kuwa mbaya zaidi katika mabasi madogo ya abiria maarufu kama Daladala,ambapo tofauti na maelekezo ya Wizara,Watetezi media imeshuhudia daladala zikiwa “Nyomi”  kama kawaida bila mamlaka yoyote inayodhibiti na kufanikisha utekelezaji wa kauli ya serikali kupitia wizara ya Afya kuwa daladala zote zibebe watu waliokaa na kuvaa Barakoa.

“Braza hawa waliosimama ndio riziki yetu,wakikaa tu tutakufa njaa,hata hela ya tajiri kwa siku haitatimia,tutaondoa magari barabarani”,amesema mmoja wa waongoza magari (Kondakta) nilipomuuliza katika kituo cha daladala cha Riverside-Ubungo,akiongoza gari lake kutoka Tabata kuelekea Makumbusho.Hali hii pia imeshudiwa katika barabara za magari yatokayo Mlonganzila,Mbezi kuelekea Manzese na mengine Makumbusho.

Kwa upande wa pikipiki,Watetezi Media imeshuhudia zile za mataili matatu (Bajaji) zikiwa hazina msongamano wa watu kama kawaida,lakini kukiwa na tatizo la abiria kutovaa barakoa,huku zile za matairi mawili (Bodaboda) zikitii agizo la kubeba abiria mmoja lakini uvaaji barakoa ukiwa songombingo.

Prof. Abel Makubi-Katibu Mkuu,Wizara ya Afya.

MWANZA

Kwa mujibu wa taarifa ambazo zilitufikia asubuhi ya leo kutoka jijini Mwanza ni kwamba suala la daladala kubeba watu waliokaa tu lilikuwa gumu wakati wa asubuhi ambapo kila mtu anataka kuwahi shughuli zake.

Mfano daladala zinazotoka Nyashishi kuelekea Igoma na Ilemela zimeonekana zikiwa na msongamano mkubwa wa watu kama kawaida ikizingatiwa uwepo wa abiria wengi eneo safari inapoanzia na pia kuwepo kwa vituo vingine vinne vinavyosubiri daladala kutoka eneo hilo kuelekea maeneo mengine ya jiji kabla ya kufika katikati ya mji,hali hiyo pia imeshuhudiwa kwa daladala zinazotoka Kisesa kwenda katikati ya mji ambapo kuna vituo viwili kabla ya kufika eneo la Igoma ambapo kuna daladala zinazoanzia safari zake pale kuelekea maeneo mbalimbali ya jiji hilo.

MBEYA

Kwa wenyeji wa mkoa wa Mbeya wanafahamu dhahiri kuwa vyombo vya usafiri si vingi sana,hivyo kila mtu huwa na haraka kutumia chombo chochote ili kuwahi majukumu yake.Licha ya mwongozo wa Wizara ya Afya kudhibiti kusambaa kwa virusi vya Covid-19,bado hadi leo asubuhi,Msongamano wa magari ulikuwa vile vile hasa katika Vituo vya Uyole kwenda Uhindini (mjini), Kabwe kwenda Uyole,Sae-Kabwe-Uyole,pamoja stendi ya Mbalizi kwenda Mbeya Mjini.

ARUSHA

Watetezi Tv pia ilifuatilia utekelezaji wa mwongozo wa Wizara ya Afya katika kudhibiti msongamano,eneo la usafirishaji katika jiji la Arusha na kushuhudia utekelezaji wa mwongozo huu ukiwa hauna usimamizi wowote na hivyo hali kuwa ya kawaida kama siku zote.Katika eneo la Kwa Mrombo,kumeshudiwa msongamano mkubwa watu wanaoshuka na kupanda kwa wingi katika magari yanayotoka  Mjini pamoja na yale yanayotoka Oljoro.Eneo jingine liliokuwa na magari yaliyobeba watu kuzidi idadi ni stendi ndogo ya Ngura kuelekea Oldonyosambu, pamoja na Sanawari Juu kuelekea mjini.

KILIMANJARO.

Huenda ndio ukawa mji pekee unaoweza kutekeleza mwongozo huu hasa kwa vyombo vya usafiri kubeba watu kadiri ya uwezo hasa katika eneo la mjini ambapo matumizi ya daladala yamepokwa na bajaji ambapo watu wanaosafiri kuelekea sehemu mbalimbali za mjini wameonekana kutumia zaidi bajaji na piki,na daladala ni nadra sana kuonekana na hata zikionekana hazina soko kutokana na uharaka pamoja na unafuu,ambapo kutoka Moshi mjini hadi Majengo ama KCMC bajaji iliyobeba watu wane hutoza kiasi cha shilingi mia tano tu.

Katika majumuisho ya taarifa hii kuhusu utekelezaji wa mwongozo wa serikali katika kudhibiti mnyororo wa usambaaji wa virusi vya Corona,kurunzi ya Watetezi Media imeona mwongozo huo katika eneo la usafirishaji hautekelezeki kirahisi hasa kudhibiti msongamano,abiria kutosimama kwenye magari (Daladala na Mwendokasi) pamoja na watu kuvaa barakoa.Haya yote bila kutumia nguvu ya ziada,hayawezekani na mapambano huenda yakawa na changamoto nyingi zaidi katika utekelezaji.