February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

JESHI LA POLISI LAZINDUA PGO YA POLISI,LSF YALIWEZESHA MIL.400

Jeshi la Polisi nchini Tanzania leo Agosti 25, 2021 limezindua mwongozo wa jumla wa utendaji kazi wa jeshi la polisi (Police General Order) baada ya kuufanyia marekebisho mapya, ambayo yanalenga kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wa jeshi hilo nchini.

Marekebisho ya mwongozo huo yanalenga kulifanya jeshi la polisi kuendelea kufanya shughuli zake kwa weledi na kuongeza uwajibikaji zaidi wa jeshi hilo katika kushughulikia masuala mbalimbali ikiwemo vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Pamoja na mambo mengine maboresho ya mwongozo huo mpya unajumuisha urasimishaji wa madawati ya kijinsia na watoto ndani ya jeshi hilo kama sehemu ya mkakati mzuri wa kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.

Kutokana na uhitaji wa maboresho ya mwongozo huo, Jeshi la Polisi nchini liliingia makubaliano na Shirika lisilo la kiserikali linalofanya kazi ya kukuza upatikanaji wa haki nchini Tanzania, Legal Services Facility (LSF), ambalo lilitoa fedha kiasi cha shilingi milioni 400 kwa ajili ya kuendesha mchakato mzima wa kupitia upya mwongozo uliokuwepo awali na kuangalia maeneo ambayo yanaweza kuboreshwa zaidi ili kuendelea kulinda na kutetea haki za wanawake na watoto nchini.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mwongozo huo, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) nchini Tanzania, Simon Sirro, amesema anayo furaha sana kushirikiana na shirika la LSF katika kufanikisha zoezi zima la kupitia na kurekebisha mwongozo wa Jeshi la Polisi nchini, ambao sasa utasaidia kuwalinda zaidi wanawake na watoto kama kundi maalum linalohitaji uangalizi kutokana na ukweli kuwa, kundi hilo ndio limekuwa likiathirika zaidi na vitendo vya ukatili nchini.

 “Ndani ya Jeshi la Polisi kuna Mtandao wa Askari Wanawake nchi nzima ambao nao umekuwa ukifanya kazi nzuri kila kukicha kuhakikisha haki na ustawi wa maendelo ya wanawake na watoto unalindwa.  Katika maboresho yaliyofanyika ya mwongozo wetu mtandao huo nao umerasmishwa pia ili kuchochea jitihada zetu pamoja kama jeshi kuendelea kulinda usalama wa raia wote hususani wanawake na watoto,” ameongeza IGP Sirro.

Kwa upande wake  Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Legal Services Facility (LSF), Lulu Ng’wanakilala amesema kukamilika kwa mapitio na maboresho ya mwongozo wa Jeshi hilo ili kusimika ama kutambua rasmi jitihada zilizokuwepo kama vile madawati ya jinsia na mtandao wa askari wanawake ndani ya jeshi hilo ni sehemu ya mkakati maalumu wa LSF kushirikiana na serikali pamoja na taasisi zake katika kufanya uchechemuzi, ili kuleta mabadiliko ya kisera, sheria na miongozo mbalimbali nchini, itakayoboresha zaidi ustawi wa haki na maendeleo ya wanawake na wasichana nchini.

“Uzinduzi huu una maana kubwa sana kwetu kama shirika binafsi linalofanya kazi ya kukuza upatikanaji wa haki nchini Tanzania.  Hii ni sehemu ya ushirikiano wetu na Jeshi la Polisi kupitia makubaliano tuliyotiliana saini ili kuweza kusaidia zoezi la kuupitia upya mwongozo wao ili kurasmisha kabisa madawati ya jinsia, ambayo yamekuwa yakifanya kazi kubwa ya kulinda na kutetea haki za wanawake na watoto nchini Tanzania.

Ng’wanakilala ameongeza kuwa mwongozo wa utendaji wa polisi ambao umeboreshwa anaamini kuwa utakwenda kusaidia watu wote hasa wanawake na watoto, ambao wamekuwa ndio kundi linalohitaji zaidi msaada wa kisheria kutokana na changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo katika maeneo mbalimbali ikiwemo nyumbani na katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Akinukuu ripoti ya LSF ya mwaka 2020, N’wanakilala amesema inaonyesha kuwa takribani watu 99,844 waliweza kupatiwa huduma za msaada wa kisheria nchi nzima, ambapo katika yao wanawake walikuwa 60,203 sawa na asilimia 60 na wanaume 39,641 sawa na asilimia 40.

“Ripoti yetu inaonyesha katika kila matukio (4) ya ukatili yaliyoripotiwa na wanawake yalihusisha unyanyasaji wa kijinsia, ambapo visa vyote vilivyoripotiwa vinakadiriwa kufikia asilimia 26.5 kwa mwaka 2020,” amefafanua Lulu Ng’wanakilala.