February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

JAMHURI YAPINGA MAOMBI YA KUBENEA YA KUMFUNGULIA KESI MAKONDA

Maombi ya Mwanahabari nguli nchini Tanzania, Saed Kubenea, ya kupata kibali cha kumgulia kesi ya matumizi mabaya ya madaraka aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, yamepingwa na Jamhuri.

Maombi hayo yaliyofunguliwa mapema mwaka huu na Kubenea, yamepingwa na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), wakidai mwanahabari huyo hana maslahi nayo.

Mapingamizi hayo yametajwa leo Ijumaa na Wakili wa Kubenea, Hekima Mwasipu, baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Subira Mwalumuli, kuieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Dar es Salaam, mbele ya Hakimu Aron Lyamuya, kwamba wajibu maombi wanakusudia kuyaleta.

Hekima Mwasipu alitaja mapingamizi mengine kuwa ni, mahakama hiyo haina mamlaka ya kuyasikiliza, sheria iliyotumika kuyafungua kutokuwa na nguvu, pamoja na maombi hayo kutokana na habari za kusikika.

Hakimu Lyamuta alipanga tarehe 29 Aprili 2022m kuwa siku ya kutaja tarehe ya utoaji maamuzi wa mapingamizi hayo.

Aidha, Hakimu Lyamuya alitoa siku 14 kwa upande wa Jamhuri, kuwasilisha hoja za mapingamizi kwa njia ya maandishi, tarehe 8 Aprili 2022.

Upande wa waleta maombi, wametakiwa kuwasilisha majibu ya mapingamizi hayo kwa maandishi tarehe 22 Aprili mwaka huu.

Kubenea amefungua maombi hayo akimtuhumu Makonda kwa matumizi mabaya ya ofisi, akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ikidai alivamia Ofisi za Kampuni ya Clouds Media Group, jijini Dar es Salaam, tarehe 17 Machi 2017.