February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

IGP SIRRO ASEMA WANAUSHAIDI WA TUHUMA ZINAZOMKABILI MBOWE

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro amewaonya baadhi ya wanasiasa, vyama vyama vya siasa na makundi mengine ya wanaharakati kutoingilia hatua zilizochukuliwa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Mendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe kwa kuwa wana ushaidi wa kutosha juu tuhuma zinazomkabili.

Amesema kuna baadhi ya wanachama wa CHADEMA wanadhani Mwenyekiti Freeman Mbowe hawezi kuhusika na aina ya tuhuma zinazomkabili, lakini amedai Jeshi hilo lina ushaidi wa kutosha.

“CHADEMA wanaona Mwenyekiti wao (Mbowe) ameonewa na wanasema hawezi kuwa hivyo wanamuona ni Malaika hawezi kufanya kosa, Kabla ya Uchaguzi nilisema kuna watu wamepanga kuhakikisha Uchaguzi haufanyiki, nilisema kuna baadhi ya watu wamepanga kulipua visima vya mafuta na kufanya mauaji ya Viongozi na nilisema tutawakamata kabla hawajafanya hivyo” amesema Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Sirro

Amesema baadhi ya watuhumiwa wengine wanaokabiliwa na tuhuma hizo amabazo zinamkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe kuwa wameshakamatwa, amedai pia kuwa jambo hilo hawezi kulizungumzia sana kwa kuwa lipo Mahakamani lakini amesisitiza kuwa Mbowe naye ni binadamu hivyo anaweza kukosea.

“Tuliwakamata kabla, hayo ya Mwenyekiti wao (Mbowe) sitaki kuzungumzia sana lipo Mahakama ila wajue yeye ni Binadamu kama Binadamu wengine na anaweza kufanya kosa tumempeleka Mahakamani tuache Mahakama itimize wajibu wake” IGP, Simon Sirro

Pia IGP Simon Sirro amesema kuwa tuhuma zinazomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA sio mpya na mtuhumiwa ambaye ni Mwenyekiti Freeman Mbowe anazijua, hivyo amewataka Watanzania kuwa watulivu kwakuwa akitumia msemo wa kiswahili usemao ‘usilolijua ni kama usiku wa giza’ ukiwa na maana waliache kwenye vyombo husika wasijiingize kwenye mtego.

“Kama kweli ni mkweli Mwenyekiti wao (Mbowe) na anamuamini Mungu waende wamuulize habari hiyo, kuna mambo unaweza kuyafanya kwamba ni siri lakini ndio mana Vyombo vya Habari vipo, niwaombe Watanzania wenzangu usilolijua ni kama usiku wa giza usiingie kwenye mtego ambao hujui aliyeutega ana jambo gani, Waende wamuulize huyo Mtu tuliyempeleka Mahakamani (Mbowe) kwamba hili jambo unalijua na kama ni ukweli ana Dini yake na anamjua Yesu Kristo aende aaambiwe” IGP, Simon Sirro

IGP, Simon Sirro hayo ameyasema wakati akizungumza na vyombo vya habari, kufatiwa kuwepo kwa baadhi ya wananchi hususani wafuasi wa CHADEMA na wanaharakati kushangazwa na tuhuma zinazomkabili Freeman Mbowe.

Ikumbukwe Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe anakabiliwa na tuhuma za Ugaidi ambapo shauri tayari limeshapelekwa Mahakamani, kwa sasa yupo Gerezani na atarejeshwa Gerezani Agousti 5, 2021.