February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

HRDC WATOA TAMKO SIKU YA KIMATAIFA YA DEMOKRASIA, YAITAKA SERIKALI KUSAINI MIKATABA INAYOLINDA DEMOKRASIA, WAKUMBUSHIA KATIBA MPYA

Onesmo Olengurumwa-Mratibu-THRDC

Na: Anthony Rwekaza

Kila Septemba 15, Dunia uadhimisha siku ya Demokrasia ambayo ilianzishwa rasmi mnamo mwaka 2007 na Mkutano wa ummoja wa Mataifa ili kuyakumbusha Mataifa umuhimu wa kusimamia mifumo na misingi ya Kidemokrasia Duniani.

Katika kuadhimisha siku hiyo leo Jumatano Septemba 15, 2021, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umeungana na Watanzania pamoja na Mataifa mengine katika kuadhimisha siku hiyo kwa kutoa tamko la kutabua Demokrasia, utawala bora na kuheshimu haki za binadamu katika nyanja mbalimbali ili kuhakikisha maendeleo ya Tanzania na watu wake vinapatikana.

Akizungumzia maadhimisho hayo Mratibu Kitaifa wa THRDC ambaye pia ni Wakili wa Mahakama kuu, Onesmo Olengurumwa amesema misingi ya demokrasia na haki za binadamu utambuliwa katika matamko na mikataba mbalimbali ya Kimataifa ikiwemo tamko la umoja wa Mataifa la mwaka 1948 kuhusu haki za binadamu na Mkataba wa umoja wa Afrika kuhusu Demokrasia, Uchaguzi na utawala wa mwaka 2007.

“Msingi wa Demokrasia na haki za Binadamu unatambuliwa katika matamko na mikataba mbalimbali ya Kimataifa ikiwemo Tamko la Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu la mwaka 1948 na Mkataba wa umoja wa Afrika kuhusu Demokrasia, Uchaguzi na Utawala wa mwaka 2007” Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa

Aidha Olengurumwa amesema kuwa Mkataba wa Afrika kuhusu Demokrasia katika Ibara ya 4 unazitaka Nchi wanachama za ummoja wa Afrika kuhakikisha kuwa zinakuza Demokrasia, misingi ya utawala wa sheria na haki za binadamu huku pia akibaisha kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania1977, Ibara ya 3 inaitaja Tanzania kuwa ni Nchi ya Kidemokrasia.

Kufuatia uwepo wa Mikataba hiyo, Mratibu huyo wa THRDC amesema Nchi ya Tanzania inao wajibu kuhakikisha kuwa Haki za Kidemokrasia na Utawala Bora vinazingatiwa, ameongeza kuwa licha ya maboresho mbalimbali yanayoendelea kufanyika kwenye sheria na mifumo ya kidemokrasia amedai bado kumekuwepo na kilio kutoka kwa wadau wa haki za binadamu pamoja na wananchi katika nyanja mbalimbali za mifumo ya kidemokrasia na utawala bora.

Ili kuboresha hali ya demokrasia na utawala bora nchiniTanzania, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania umetoa mapendekezo kwa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumzia mapendekezo hayo Wakili wa Mtandao huo Leopord Moshi, amesema THRDC inaishauri Serikali ikubali kutia saini Mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda inayohusiana na demokrasia, ikiwemo Mkataba wa Umoja wa Afrika Kuhusu Demokrasia, Uchaguzi na Utawala wa mwaka 2007.

Lakini pia Wakili huyo amesema wanaitaka Serikali kusimamia misingi ya kidemokrasia na haki za binadamu kama ilivyohainishwa kwenye Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na mikataba ya kikanda na kimataifa.

Katika hatua nyingine THRDC imeishauri Serikali izingatie kanuni na sheria zinazoendana na misingi ya kikatiba ili kuhakikisha kuwa utawala wa sheria unatamalaki katika nchi ya Tanzania huku wakiitaka Serikali iweke mifumo bora itakayowezesha ushiriki wa Watetezi wa Haki za Binadamu na wananchi wote kuweza kushiriki katika chaguzi na michakato mingine ya kidemokrasia.

Katika hatua nyingine Afisa Uchechemzi wa THRDC, Nuru Malo kwa niaba ya mtandao huo Serikali ya Tanzania ifikirie upya uamuzi wake wa kuzuia wananchi na mashirika yasiyo ya kiserikali kufungua kesi katika mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu.

Vilevile Afisa huyo ameongeza kuwa wanaishauri Serikali kusikia kilio cha wananchi kuhusu kukamilisha mchakato wa katiba mpya, huku akipendekeza Serikali ijenge dhana ya kushauriana na kujadiliana na makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na makundi ya kidini, Asasi za Kiraia, Sekta binafsi na wananchi kwa ujumla.

Maadhimisho hayo mwaka huu (2021) yamebebwa na kauli mbiu isemayo ‘Kuimarisha Uthabiti wa Kidemokrasia pindi Changamoto zinapotokea’.

Ikumbukwe Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu kupitia wanachama wake kwa mara tofauti wamekuwa wakikemea vitendo mbalimbali ambavyo wamekuwa wakivitafsiri kama uvunjifu wa haki za Binadamu na pia wamekuwa wakiwezesha jamii kutambua mambo mbalimbali yanayogusa Haki za Binadamu ikiwa ni sehemu ya Demokrasia.

MWISHO…