February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

HISTORIA YAANDIKWA;MTANDAO WA KUTETEA WANAWAKE WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU WAZINDUA MPANGO MKAKATI WA KWANZA

Mtandao wa Wanawake Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (CWHRDS) hii leo umezindua Mpango Mkakati wake wa Kwanza wa miaka mitano (2022-2026) ambapo kiasi cha takribani Bilioni 1 kinakusudiwa kutumika katika utekelezaji wa Mpango huo wa miaka mitano.

Akizungumza wakati wa Uzinduzi uliofanyika katika Hoteli ya Four Points,Jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Mtandao huo,Hilda Stuart  amesema dira ya Mtandao huo ni kuhakikisha kunakuwepo na mazingira salama kwa wanawake watetezi wa haki za binadamu nchini Tanzania.

“Kama Mtandao wa Wanawake Watetezi wa haki za binadamu hapa Tanzania tumekuwa tukifanya kazi kwa matukio lakini sasa tukaona jinsi tunavyokuwa tunahitaji kuwa na dira,cha kwamza tumelenga kabisa kutengeneza mazingira salama ya wanawake watetezi wa haki za binadamu ili wanapofanya kazi zao za utetezi wawe kwenye mazingira ambayo yanakuwa na ulinzi,”amesema.

Aidha ameongeza kuwa licha ya wanawake watetezi wa haki za binadamu kuwa mstari wa mbele katika kufanya shughuli mbalimbali za utetezi wa haki za binadamu lakini hakuna sheria zinazowafanya wafanye kazi zao katika mazingira salama.

“Mikataba ya kimataifa inasema kwamba nchi inatakiwa itoe ulinzi kwa Wanawake watetezi wa haki za binadamu kwasababu wanawake watetezi wa haki za binadamu wanafanya kazi kubwa sana lakini cha kushangaza hakuna zile ‘mechanism za kuwafanya wafanye kazi katika mazingira salama’,”ameongeza Hilda.

Pia amesema eneo linguine ambalo watalifanyia kazi kupitia Mpango Mkakati huo ni wao wenyewe kujiweka imara katika kufanya kazi zao za kiutetezi kama wanawake.

“Wanawake tumekuwa wahanga wakubwa wa masuala ya ukatili wa kijinsia kwasababu tu sisi tulivyo na mifumo dume,na kwakuwa ninatetea mwanamke mwenzangu lakini jamii inakuja na yenyewe inaniattack,”amesema Hilda huku akitilia mkazo wa kuwepo kwa kesi Zaidi ya tano ambapo wanawake watetezi wametetea katika kesi mbalimbali lakini wanafamilia wamekuwa wakiwatishia.

Kwa upande wake Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC),Onesmo Olengurumwa amesema THRDC imefarijika kuona kuna Mtandao mwingine ambao upo kwa ajili ya kulinda na kutetea maslahi ya wanawake watetezi wa haki za Binadamu

“Ni jambo ambalo tunafarijika kwamba leo wanawake wanafika mahala wanazindua Mpango Mkakati wa namna ya kulinda na kutetea haki za Binadamu hususani haki za wanawake na watoto kama  wanawake watetezi hapa nchini,”amesema Olengurumwa.

“Mpango huu wa miaka mitano umejikita Zaidi kuwajengea uwezo wanawake lakini kuweka mazingira mazuri ya watetezi wanawake wanaotetea haki za binadamu lakini pia Zaidi haki za wanawake na watoto waweze kuwa katika mazingira mazuri sana ya utetezi wa haki za wanawake hapa Tanzania,”

Aidha ameongeza kuwa THRDC kama Mtandao mama utaendelea kutoa ushirikiano wake kwa Mtandao huo wa wanawake Watetezi wa Haki za Binadamu nchini.

“Ni furaha kwetu na faraja na tunaendelea kushirikiana sisi kama THRDC tuna miaka 10 sasa tutaendelea kuwa sehemu ya kushirikiana nao  katika kuhakikisha wanafanikiwa wanafikia malengo yao,”

Naye Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika masuala ya Wanawake nchini Tanzania,Hodan Addou ameupongeza Mtandao huo kwa kazi kubwa inayofanya katika kutetea masuala ya wanawake watetezi wa haki za Binadamu na kuahidi kuwa kama UN-Women wataupitia Mpango Mkakati wao na kuona namna watakavyoshirikiana katika kutekeleza malengo ya Mtandao huo kwa miaka mitano ijayo.

Mtandao wa Wanawake Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania ulianzishwa takribani miaka mitatu iliyopita kwa lengo la kuhakikisha inawaleta pamoja  wanwake watetezi wa haki za Binadamu  na kuweza kulinda maslahi yao lakini pia kuwajengea uwezo ili waweze kufanya kazi kubwa ya utetezi wa haki za binadamu nchini.