February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

HAYA NDIYO MAPENDEKEZO YA WANANCHI WA LOLIONDO YALIYOWASILISHWA KWA WAZIRI MKUU

Hivi karibuni Kamati Maalum ya kukusanya mapendekezo na maoni ya wananchi kuhusu mgogoro wa ardhi unaondelea Wilayani Ngorongoro mkoani Arusha iliwasilisha ripoti ya mapendekezo hayo kwa serikali,ripoti ambayo ilipokelewa na Waziri mkuu, Kassim Majaliwa.

Katika andiko hilo lenye kurasa 133 LA Ripoyi ya Mapendekezo ya Wananchi juu ya utatuzi wa mgogoro wa ardhi Tarafa ya LKolionod na Sale ,Wananchi hao wameiomba Serikali ilitambue eneo lenye kilomita za mraba 1500 katika Tarafa za Loliondo na Sale kuwa ni eneo halali la Vijiji kwa mujibu wa sheria na kubainisha kuwa wananchi wa eneo hilo wapo tayari kujadiliana na serikali katika kutafuta suluhu ya kudumu mgogoro  huo uliodumu kwa zaidi ya miongo mitatu.

“Chanzo kikuu cha mgogoro huu kati ya wananchi na Wizara ya Maliasili na Utalii kimesababishwa na kuchochewa na Kampuni ya OBC, hivyo ili kuishi kwa amani katika Vijiji vyetu na kuendelea kuwa na mahusiano mazuri na Serikali yetu, kampuni hii iondolewe katika eneo hili la Tarafa za Loliondo na Sale ili tupate nafasi huru ya kujadili swala la uhifadhi na maendeleo ya wananchi kwa kushirikiana na Serikali yetu”imeanisha Ripoti hiyo.

Aidha katika mapendekezo yao,wakazi hao wameiomba serikali Kufanya mapitio ya mipango ya matumizi ya ardhi ya Vijiji ili kukidhi mahitaji ya sasa ya kijamii, kiuchumi, kimazingira nakiutawala kwa Mujibu wa Sheria za Mipango ya Matumizi ya Ardhi Na. 6 ya 2007 na Sheria ya ardhi ya Vijiji Na.5 ya 1999.

Pia, wameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii isitishe azma ya kumega sehemu ya ardhi ya vijiji kwa matumizi ya uhifadhi na uwindaji kwani eneo hili ni ardhi halali ya Vijiji husika.

“Serikali itambua na kuendeleza uhifadhi wa kijamii kwa malengo ya kulinda rasilimali asili pamoja na haki za ardhi wafugaji” imesema.

Kwa upande mwingine Ripoti hiyo ya wananchi imeainisha kuwa eneo hilo la kilomita za mraba 1500 za Tarafa ya Loliondo na Sale ni eneo linalotegemerwa kiuchumi na wakazi 66,000 hivyo kupoteza ardhi hiyo kutawarudihsa wananchi katika wimbi la umasikini na ufukara.

“Serikali ikatae pendekezo la kumegwa kwa eneo la ardhi ya Vijiji vya Loliondo na Sale lenye ukubwa wa kilomita za mraba 1500 na eneo la Ziwa Natron inayojumuisha Kata za Pinyinyi na Engaresero kwa lengo la kuingizwa kwenye eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCA) kama ilivyopendekezwa na Kamati ya wahifadhi ya matumizi mseto ya ardhi yaani Multiple Land Use Model (MLUM) ya 2019,” imeongeza

Ripoti hiyo imeeleza kuwa wakazi wa Tarafa ya Loliondo wanategemea eneo hilo kwa zaidi ya asilimia 90 kufanya shughuli za ufugaji asilia kama chanzo kikuu cha mapato na chakula na kuiomba serikali isitambue eneo hilo kuwa ni la wazi bali nyanda za malisho, pamoja na kutilia maanani shauri la mgorogor huo ambalo kwa sasa lipo katika mahakama ya haki ya Afrika Mashariki.

“Tunaisihi Wizara ya Habari na Mamlaka ya Mawasiliano nchini kupiga marufuku vyombo vya habari visivyo fuata maadili ya uandishi ambyo vinatoa taarifa za uongo, upotoshaji na uchonganishi kati ya serikali na wananchi wa Tarafa za Loliondo na sale” imeongeza

“Tunashauri Serikali itambue haki za mashirika na watetezi wa kijamii na haki za binadamu ambao wamekuwa wakisumbuliwa mara kwa mara wanapojaribu kusaidia serikali na jamii kutatua changamoto hizi,”

Aidha wameiomba Serikali ipige marufuku kamata kamata ya viongozi wa kijamii inayoendelea kwa sasa katika Tarafa za Sale na Loliondo kwani kitendo hicho kinaendelea kuzua taharuki miongoni mwa jamii na kufifisha jitihada za pamoja za kutatua changamoto hizo.

Pi ripoti hiyo imependekeza kuundwa kwa Tume Huru itakayochunguza  ukiukwaji wa haki za binadamu na haki za wafugaji zilizofanyika kwa kipindi cha miaka 30 iliyopita katika eneo hilo lenye mgogoro.

“Tunapendekeza kuwa kuanzia sasa swala la mgogoro wa Loliondo na Sale uwe unakwenda kwa njia ya mazungumzo kupitia kamati hii ya jamii pamoja na serikali il kupunguza mivutano isiyokuwa ya lazima. Kamati hii itasaidia kuondoa mwanya wa watu wasiohusika na mgogoro huu na wanaotoka nje ya Wilaya ya Ngorongoro kutumika katika majadiliono ya kutatua mgogoro huu,”imesema Ripoti hiyo.

“Kwa kuzingatia kuwa nchi ipo katika uchumi wa kati, serikali iboreshe na kufungua fursa mbali mbali za kibiashara kwa kuboresha miundo mbinu hasa masoko, Kiwanda cha kuchakata mazao ya mifugo, elimu za ufugaji wenye tija, mtandao wa barabara za lami nk. Hatua hii itatoa fursa kwa wananchi kupata fursa za kimaendeleo kwa haraka na kuchangia pato la taifa pamoja na kupunguza migogoro ya rasilimali”

Aidha Ripoti hiyo imependekeza kuwa Serikali ifanye jitihada za haraka kuwekeza katika Elimu  na kuendeleza watoto wa jamii hiyo ya kifugaji ikiwemo kujenga shule za msingi katika kila kitongoji kilichopo Zaidi ya kilomita 7 kutoka kitovu cha Kijiji.

Ripoti hiyo ya wananchi kuhusu mgogoro wa ardhi katika Trafa ya Sale na Loliondo imelezaa kwa kina kuhusu chanzo cha mgogoro huo wa muda mrefu wa ardhi katika maeneo ya kata Nane za Loliondo na Sale zinazopakana na Hifadhi ya Serengeti.