February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

HATIMAYE NYUMBA ZA POLISI ZILIZOKAMILIKA TANGU 2019 ZARUHUSIWA KUTUMIKA.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi George Simbachawene ameruhusu askari Polisi kuanza kutumia nyumba za kisasa zenye uwezo wa kubeba familia zaidi ya 300 zilizopo katika eneo la Kunduchi na Mikocheni jijini Dar es salaam.

Waziri Simbachawene amesema hayo leo wakati alipofanya ziara ya kikazi na kukagua Mradi wa nyumba za kisasa za makazi ya askari ambapo ameelekeza kutumika kwa nyumba hizo ambapo kutasaidia kupunguza uhaba wa nyumba za askari na kuleta ufanisi kwa askari wanapotekeleza majukumu yao ya kazi za Kipolisi.

“Kinachendelea hapa ni hasara,nyumba zinaendelea kuchakaa,majani yanaota mpaka ndani ya nyumba kwa sababu hakuna watu wanaishi” ameshangaa Waziri Simbachawene na kuongeza neno “Nyumba ni Tamu” baada ya kuingia ndani na kuona ubora wa nyumba hizo.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro amesema tangu kukamilika kwa mradi huo imepita miaka mitatu hadi sasa jambo ambalo linapelekea kuharibika kwa baadhi ya sehemu za nyumba hizo kwa kukosa matunzo kwa kutokutumiwa na askari wa Jeshi hilo.

“Kwa utendaji wa polisi wanapoona namna hiyo,na walishaondolewakwenye nyumba zao na kuahidiwa kurudishwa kwenye zao halafu hawaoni wanarudishwa,tunapata sana shida kusimamia askari”,amesema IGP Simon Sirro.

Hata hivyo wakuu hao hawakuweka bayana sababu za askari kutohamia katika nyumba hizo hata baada ya kukamilika  miaka mitatu iliyopita.