February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

HATIMA KESI YA MBOWE KUJULIKANA SEPTEMBA 6.

Na Leonard Mapuli.

M/Kiti wa CHADEMA Freeman Mbowe akiwa Mahakamani September 3.

Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu uchumi imeiahirisha hadi Jumatatu,September 6,ambapo itatoa uamuzi wa pingamizi za mapungufu kisheria,yaliyowasilishwa Mahakamani hapo na mawakili wa utetezi,katika kesi ya Uhujumu uchumi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Upinzani nchini Tanzania.Freeman Mbowe na wenzake watatu.

Awali, Jopo la mawakili wa Mbowe likiongozwa na wakili maarufu Peter Kibatala,liliiomba mahakama kumuachilia huru Mbowe na wenzake kwa kuwa mahakama hiyo haina mamalaka kisheria kusikiza kesi hiyo.

Upande wa utetezi umeweka mapingamizi kadhaa ya kesi hiyo kutosikilizwa katika mahakama Kuu,divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi  kwani kwa  mujibu wa sheria ya kuzuia ugaidi kesi hiyo inapaswa kuskilizwa na mahakama kuu ya kawaida na si divisheni maalum iliyoanzishwa kwa ajili ya makosa ya rushwa na uhujumu uchumi.

Mawakili wa Serikali,leo September 03,waliwasilisha mahakamani hapo utetezi dhidi ya pingamizi iliyowekwa na upande wa mawakili wanaomtetea Mbowe,waliowakilisha mapingamizi matatu mnamo September 1,ikiwa ni pamoja na hati ya mashitaka kukosa viashiria vya makosa na kushtaki watuhumiwa kwa kosa la kula njama pamoja na makosa mengine kinyume na utaratibu wa kuandaa hati ya mashtaka,ambapo upande wa Jamhuri leo ulikuwa na kibarua cha kupangua hoja za upande wa pili katika shauri lilisikilizwa kwa muda wa masaa 9,kuanzia Saa tatu asubuhi,huku mahakama ikilazimika kutoa mapumziko ya dakika 30 kabla ya kuendelea kusikiliza hoja za serikali.

Baada ya kusikia hoja za serikali za kwa nini kesi hiyo isiondolewe mahakamani hapo,Jaji anayesikiliza kesi hiyo,Eliezer Luvanda,ameomba muda kupitia hoja zote,na kwamba Jumatatu,September 6,Mahakama hiyo itatoa maamuzi ya pingamizi zilizowekwa na upande wa utetezi.

Mbowe,akiwa na viongozi wengine 10 wa Chadema,walikamatwa Julai 20,wakiwa katika Hoteli moja jijini Mwanza,baada ya askari polisi kufika eneo hilo na kuwachukua kwa nguvu,siku moja kabla ya Kongamano la Kudai Katiba mpya lilokuwa limepangwa kufanyika jijini humo,Julai 21.Hata hivyo Mbowe alisafirishwa kutoka Mwanza hadi Dar es Salaam,huku viongozi wengine wa Chadema akiwemo mbunge wa zamani wa Tarime vijijini John Heche,wakibaki rumande kwa siku kadhaa kabla ya polisi kuwaachia huru bila kusomewa mashtaka yotote.