February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

GIZA BADO NENE MAUAJI YA MTENDAJI MBEZI

Na Leonard Mapuli.

Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam Amos Makala amesema,watu wawili wametiwa nguvuni,wakihusishwa na mauaji ya kinyama ya Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Mbezi Msumi,aliyeuawa Jumatatu ya Oktoba 11, (Jana),kwa kuvamiwa na watu waliokuwa wameficha silaha,waliofika ofisini kwake,na kuomba kupatiwa huduma za kiofisi kabla ya kuanza kumshambulia hadi umauti.

Kwa mujibu wa mashuhuda,watu hao walifika ofisini kwa Mtendaji na kumkuta akiwa peke yake,wakati ambao wahusika wengine wa ofisi hiyo wakidaiwa kwenda kwenye majukumu mengine,huku mlinzi wa ofisi hiyo pia akidaiwa kwenda mghahawani kujipatia kifungua kinywa.

Katika eneo la Msumi,hali ya taharuki imeendelea kutamalaki kufuatia mauaji hayo yaliyofanyika mchana kweupe ambapo hadi sasa chanzo chake hakijawekwa bayana,huku jeshi la polisi likiarifu kuendelea na upelelezi wake.

Asubuhi ya leo (Oktoba 12),Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salamu amefika eneo la tukio akiongozana na kamati ya ulinzi na usalama,Kisha baadae akaelekea nyumbani kwa wazazi wa Marehemu Kelvin,eneo la Mbezi Makonde,ambako taratibu za maziko zinafanyika.Akiwa nyumbani hapo,amewafariji wafiwa waliokusanyika kuomboleza,pamoja na kueleza kuwa Serikali imeshakamilisha taratibu zake na kwamba familia inaweza kuendelea na taratibu za mazishi.

Baadhi ya Watendaji mbalimbali wa Mitaa waliozungumza na Watetezi Tv,wameonesha hofu baada ya mauaji hayo,na kuwa yasipodhibitiwa,watashindwa kufanya kazi zao kwa ufanisi,na wameiomba Serikali kuwaimarishia ulinzi Katika maeneo yao ya kazi, ambapo wamekuwa wakipambana na changamoto za kiusalama kufuatia wingi wa migogoro inayoripotiwa Katika ofisi zao.