December 4, 2022

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

GENGE LA VIJANA WA KISUKUMA KATAVI LAFUMWA LIKIFANYA “CHAGULAGA”.

Vijana wa Kabila la Kisukuma,waliofumwa Wakifanya "Chagulaga",Januari 13 Wilayani Mlele-Katavi.

Na Leonard Mapuli-lennymapuli@gmail.com/Picha:Eden Ezekiel Wayimba

“Chagulaga” (Chagua) ni mila  iliyokuwa ikifanywa na watu wa kabila la wasukuma,ambapo kundi la vijana kuanzia watano hadi kumi,wenye umri tofauti,walikuwa wakigombea msichana mmoja,wote pamoja wakimshika katika sehemu mbalimbali za mwili wake,kila mmoja akimvuta awezavyo,ili kuwashinda wenzake,na hatimae kuondoka nae.

“Chagulaga” ilikuwa ikifanyika katika maeneo mbalimbali ambayo yana mkusanyiko wa watu,waliofika kwa wingi,kutoka maeneo ya mbali,kwa shughuli maalumu kama vile maonesho ya Ngoma,Minada,Masoko,ama sherehe za kitamaduni.Lakini ilikwenda mbali Zaidi ambapo wanaume mara nyingine walilazimika kuwafuata wanawake,katika sehemu za mawe maalumu ya kusaga nafaka ili kupata unga.Hapo wanaume walifika ni kumchagua mwanamke ama binti aliyekuwa anasaga unga kwa umaridadi mkubwa,na kuanza kumtongoza.

Kwa wanaume waliokuwa wakishiriki chagulaga kupitia maonesho ya Ngoma,Minada,Masoko,ama sherehe za kitamaduni,ilikuwa ni lazima kwao kuwasubiri mabinti barabarani,pindi wanaporudi kutoka kwenye matukio hayo,na kisha kuanza “Chagulaga” kwa kuwakimbiza barabarani na kisha kuwakamata,na kuwalazimisha kuchagua mwanaume kwa nguvu.

Katika zoezi hilo,busara za msichana ndizo zilihitajika ili kumnusuru,na kitu pekee ambacho kilikuwa msaada kwa msichana,ilikuwa ni yeye mwenyewe kwa hiari kuchagua mwanaume mmoja kati ya hao wengi,kwa kumshika mkono,kitendo ambacho kwa mila hiyo,kilitosha kuwafanya wanaume wengine wote kusambaa,na kumuacha aliyeshikwa mkono kuendelea na mazungumzo na msichana.

Mazungumzo yaliyokuwa yanafanyika baada ya “Chagulaga” yalikuwa ni ya mapenzi.Mwanaume alipata muda wa kumtongoza mwanamke,na walipokubaliana,basi walianzisha penzi siku hiyo hiyo hiyo,na waliposhindwa kukubalian,ulikuwa ndio mwisho,japo baadhi ya wanaume walilazimika kumbaka binti kabla ya kuachana,zoezi ambalo lilikuwa maarufu kwa jina la “Kupondya”,yaani kumlaza chini mwanamke kwa nguvu,na kisha kumbaka.

Wasichana waliokuwa wakihusika katika “Chagulaga” ni wale wa chini ya miaka 18, huku wengine wakiwa ndio kwanza wamevunja ungo,huku pia vijana waliokuwa wabalehe wakiwa wahusika wakubwa katika mchezo huo.

Wanaharati wa masuala ya haki za Binadamu waliilamikia mila hii,pamoja na zingine nyingi kama Nyumba Ntobhu,Urithi wa wake,ukeketaji,na nyingine nyingi,kuwa zilikuwa kinyume na Haki za Wanawake wa Wasichana,na serikali ilipiga maarufuku mila hizi ambazo pamoja na madhara mengine,zilikuwa wakala mkubwa wa kusambaza na kueneza virusi vya Ukimwi,pamoja na mimba za utotoni.

“Vijana wakigombea Msichana (Chagulaga) wilayani Mlele,Januari 13,2022-Picha na Eden Ezekiel Wayimba.

Katika hali isiyo ya Kawaida,mnamo Januari 13 mwaka huu, Shuhuda wa Watetezi Tv,alishuhudia genge la Vijana wa jamii ya kisukuma, katika kata ya Chamalendi,Wilayani Mlele mkoani Katavi, wakigombea wasichana wadogo barabarani,katika zoezi la “Chagulaga”,linaloonekana kushamiri na kuendelezwa katika eneo hilo.

Video iliyorekodiwa na shuhuda,inayopatikana katika Ukurasa wetu wa Twitter na Facebook,ni uthibitisho kuwa,bado nguvu kubwa inahitajika,ili kutokomeza vitendo vya udhalilishaji kwa wasichana na wanawake,vinavyoendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini,licha ya kupigiwa kelele na wanaharakati,pamoja kupigwa vita na mamlaka za serikali.