February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

DPP AMFUTIA MASHTAKA KIGOGO CHADEMA, ALIYEDAIWA KUMUITA IGP SIRRO GAIDI, FISADI

 

Na: Anthony Rwakaza

Mkurugenzi wa Mashitaka nchini Tanzania (DPP), Sylvester Mwakitalu leo Jumatano Feburuari 23, 2022 amemuomdolea mashitaka ya uchochezi yaliyokuwa yanamkabili Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Chadema (BAZECHA), Hashimu Juma, kupitia kifungu cha 90 (1), katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es salaam.

Itakumbukuwa OKtoba 07, 2021, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Chadema (Bazecha) Hashimu Juma Issa (63) alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashitaka mawili, likiwemo la kuchapisha taarifa za uongo na kuzisambaza kwenye mtandao wa YouTube.

Mshtakiwa huyo alifikishwa Mahakamani kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es salaam ambapo alisomewa mashitaka hayo na Wakili wa Serikali, Yusuph Abood mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rashid Chaungu.

Wakili Abood ambaye aliwakilisha upande wa mashtaka aliileza mahakama kuwa Oktoba 1, 2021 katika eneo la Kinondoni B, mtaa wa Ufipa, mshtakiwa alisambaza taarifa kwa lengo la kumchafua na kumdhalilisha Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro.

Katika maelezo yake Wakili huyo alidai kuwa mshtakiwa alichapisha kwenye kompyuta na kusambaza taarifa kuwa IGP Sirro ni gaidi namba moja nchini Tanzania na ni fisadi.

Pia katika shtaka lingine ni kuwa tarehe hiyo hiyo (Oktoba 1, 2021) katika eneo la Kinondoni B, mtaa wa Ufipa, mshtakiwa alitoa maneno ya uchochezi alizozielekeza kwa IGP Sirro kuwa zilikuwa na lengo la kutengeneza chuki kwa wananchi, lakini mshitakiwa huyo alikana mashtaka hayo.

Aidha kufuatia kuelezwa mbele ya Mahakama kuwa uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo haujakamilika, Mahakama ilimuachia Mshtakiwa huyo kwa dhamana kwa masharti yaliyomuitaji kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh3 milioni kila mmoja, sambamba na barua ya utambulisho pamoja na kitambulisho cha taifa.

Juma Isaa ambaye ni mjumbe wa kamati kuu ya Chadema alidaiwa kukamatwa Oktoba 3,2021 mjini Unguja, Zanzibar kisha kushikiliwa kwa muda kabla ya kusafirishwa kuletwa kwenye Dar es Salaam kwa mahojiano zaidi.