February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

DPP AIONDOA KESI YA ABDUL NONDO KATIKA MAHAKAMA YA RUFANI

Mkurugenzi wa Mashitaka nchini DPP amewasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi ya Rufaa namba 30 ya mwaka 2022 inayomkabili Abdul Omary Nondo.

Hayo yameelezwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi,Basilius Namkambe wakati rufaa ya kesi hiyo ilipotajwa kwa kusikilizwa katika Mahakama ya Rufani masijala ya Iringa.Hivyo mahakama imeifuta kesi hiyo.

Mnamo Mei 11, 2020, Mkurugenzi wa Mashtaka alikata rufaa katika Mahakama ya Rufani ya Tanzania baada ya kutoridhishwa na uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania uliompa ushindi Nondo.

Machi 6, 2018 majira ya saa sita usiku Abdul Nondo alitekwa na watu wasiojulikana katika eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam, Tanzania. Hata hivyo, alifanikiwa kutuma ujumbe kwa rafiki yake Paul Kisabo kwamba “am at risk”, akimaanisha niko hatarini.

Tarehe 7 Machi, majira ya saa12 jioni alikutwa Mafinga, Mkoani Iringa. Nondo aliripoti tukio hilo katika kituo cha polisi cha Mafinga kuwa alitekwa na watu wasiojulikana katika eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam na alitelekezwa eneo la Mafinga, Iringa.

Baada ya kuripoti katika kituo cha Polisi Mafinga, aliwekwa ndani na kushikiliwa kwa muda wa siku 14 kabla ya kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa tarehe 21 Machi 2018 na kusomewa mashtaka ya kuchapisha taarifa za uongo (“am at risk”) kinyume na Kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 na kutoa taarifa za uongo kwa mtu aliyeajiriwa katika utumishi wa umma (Afisa wa Polisi) kinyume na kifungu cha 122 (a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Mawakili wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Bw. Jebra Kambole na Chance Luoga walisimamia kesi hiyo na Bw. Abdul Nondo alishinda kesi hiyo na kuachiwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa, na Mahakama Kuu ya Tanzania tarehe 23 Desemba 2019.

Mkurugenzi wa Mashtaka hakuridhishwa na uamuzi wa Mahakama Kuu, hivyo alikata rufaa hii ya pili. Abdul Nondo atawakilishwa na mawakili: Jebra Kambole, Chance Luoga na Paul Kisabo kutoka Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu.

Abdul Nondo alikuwa Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP) wakati anatekwa na kwa sasa ni Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja wa Vijana wa Chama cha ACT Wazalendo