February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

DKT. GWAJIMA AMKINGIA KIFUA MAGUFULI KUHUSU KUKATAA CHANJO YA CORONA.

Rais Samia Suluhu akichomwa Chanjo dhidi ya Covid-19-Picha:Watetezi Tv

Na Leonard Mapuli

Waziri wa Afya Dkt.Doroth Gwajima amemkingia kifua aliyekuwa Rais wa Tanzania,Hayati Dkt. John Magufuli kuwa hakukataa chanjo dhidi ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Covid-19 na kwamba alitafsiriwa vibaya katika kauli yake aliyoitoa akiwa Chato,kuhusu chanjo ya ugonjwa huo.

Mnamo Januari 27 mwaka huu,akiwa Chato,Hayati Magufuli aliipa rai wizara ya Afya kutokuwa na wepesi wa kukimbilia kile alichokiita “Machanjo” bila yenyewe kujiridhisha,kauli ambayo ilitafsiriwa kuwa kiongozi huyo hakuwa na imani na chanjo dhidi ya virusi vya Corona ambayo ilikuwa tayari imeshaanza kutolewa katika baadhi ya mataifa duniani.

“Wametokea sasa wataalamu,wa kuhariri hii hotuba,na kujikita katika hicho kivuli,na kupotosha,halafu wametokea wasikilizaji wakishasikiliza hicho kitu kikishapelekwa,wanaenda nacho kuwapotosha wengine,ndugu zangu watanzania,hili jambo siyo zuri,ndugu zangu wanahabari,hili jambo siyo zuri”,amesema Dkt Gwajima na kuomba hotuba za viongozi ziheshimiwe huku akilaani alichokiita upotoshaji juu kauli ya Hayati Magufuli.

Dkt.Doroth Gwajima-Waziri wa Afya.(Picha:Watetezi Tv)

Kauli ya waziri huyo maarufu ameitoa katika hotuba yake kwenye  uzinduzi wa chanjo ya Corona uliofanyika Ikulu ya Dar es Salaam,ambapo Rais wa Tanzania Samia Suluhu alizindua chanjo hiyo na kuwa wa kwanza kuchanjwa tangu serikali yake iliporuhusu watanzania kupatiwa chanjo hiyo kwa hiari.

Katika hotuba yake kabla ya kupatiwa  chanjo,Rais Samia amezishukuru Wizara ya Afya  na ile ya Mambo ya Nje, kwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha Tanzania kama taifa,kwa kupitia wahisani mbalimbali ndani na nje ya nchi,inafanikiwa kuwanusuru raia wake dhidi ya janga hilo lililoitikisa dunia na kusababisha vifo zaidi vya watu zaidi ya milioni nne kote duniani,na kuathiri uchumi wa dunia kwa ujumla.

“Nishukuru kwamba juzi (Jumapili Julai 25),kupitia Ubalozi wa Marekani, tumeweza kupokea chanjo hizi milioni moja na maelfu kadhaa,ambayo leo baada ya kuthibitishwa na wizara ya Afya,leo tunaanza kuchanja”,amesema Rais Samia Suluhu Hassan,mwanzoni wa hotuba yake.

Tangu kuwasili kwa chanjo hiyo hapa nchini,kumekuwa na mjadala mzito,wengine wakisema inaweza kuwa na madhara kiafya siku za usoni kwa watakaochanjwa,  ama kizazi kijacho,mjadala ambao umechagizwa zaidi na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima,Josephat Gwajima,ambae kupitia video zake zilizosambaa na kutazamwa sana mitandaoni ,akisisitiza kuwa ataendelea kushikilia  uliokuwa msimamo wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati Dkt. John Magufuli,kwa kukataa chanjo wala kuvaa barakoa,na kwamba ugonjwa huo utaondoka kwa maombi.Hata hivyo kauli ya kiongozi huyo wa dini imekwenda tofauti na utetezi uliotolewa na waziri wa Afya Dkt. Gwajima aliyekanusha kuwa hayati Magufuli hakukataa chanjo.

Askofu Josephat Gwajima akiwa na Hayati Magufuli enzi za Uhai wake.

Mjadala juu ya kuchanjwa ama kutochanjwa umeendelea kuwa gumzo hasa vijiweni na mitandaoni ambapo kuna kundi la watu limebaki njia panda lisijue nini cha kufanya,kutokana kelele kuwa nyingi,ambazo pia huenda zikawapa hofu wananchi wengi licha ya Rais Samia kuonesha njia kwa yeye kuwa wa kwanza kuchomwa chanjo hiyo hadharani.

“Toka nimeanza kuzungumza jambo hili la chanjo,kama alivyosema waziri,kuna wengi wanalikataa,lakini wengi sana wanalikubali”,amesema Rais Samia Suluhu na kuongeza kuwa,chanjo ni hiari,na chanjo ni imani ambapo amewataka wote wanaohiari ama wenye imani nayo wasisite kupatiwa kwani haina madhara.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya,chanjo hiyo aina ya Johnson&Johnson (J&J) itatolewa mara moja tu kwa kila atakayepatiwa,na haina awamu tofauti kama chanjo zingine ambazo mtu angehitaji kupatiwa zaidi ya mara kadhaa.

Wengine waliopatiwa chanjo hiyo katika siku ya kwanza ni pamoja na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma.baadhi ya mawaziri,Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,wakuu wote wa wilaya za Dar es Salaam,Viongozi wa dini,na makundi mengine yaliyofika Ikulu ya Dar es Salaam kushuhudia uzinduzi wa chanjo hiyo.