March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

DC KILINDI AJITOSA MGOGORO WA WAFUGAJI,WAKULIMA-LENGUSERO

Sauda Mtondoo-Mkuu wa Wilaya ya Kilindi.

Na Leonard Mapuli.

Mkuu wa wilaya ya Kilindi mkoani Tanga  Sauda Mtondoo ameahidi kufuatilia mgogoro wa wafugaji na wakulima katika kijiji cha Lengusero wilayani humo unaofuka chinichini na kufanya hali ya usalama baina ya makundi hayo mawili kutia shaka kufuatia utegwaji wa mifugo na kukata mapanga mifugo na kujeruhi wachunga mifugo silaha za jadi, unaodaiwa kufanywa na wakulima pindi wafugaji wanapopitisha mifugo jirani na mashamba huku mkulima mmoja ambae si mkazi wa kijiji hicho akidaiwa kushambulia mifugo kwa bunduki aina ya gobole.

Katika mahojiano maalumu na Watetezi TV ofisini kwake,Mkuu huyo wa wilaya amekiri kuwepo kwa migogoro mingi katika maeneo mbali mbali ya wilaya ya Kilindi yanayochangiwa na sababu nyingi zikiwemo utata katika mpango wa matumizi ya ardhi,wafugaji na wakulima kuongezeka,pamoja viongozi wa mila.

Awali kabla ya mahojiano na mkuu huyo wa wilaya,Watetezi Tv ilifika katika kijiji cha Lengusero na kushuhudia wingi wa mashamba makubwa hasa ya mahindi yaliyopo karibu na mahali pa kupitisha mifugo,na kujionea mifugo inayodaiwa kukatwa miguu na wafugaji,ama kujeruhiwa katika sehemu mbali za miili. Ilishuhudiwa  pia vijana wengi wakichunga mifugo wakiwa wamejihami kwa silaha za jadi, pamoja na uharibifu mkubwa wa mazingira uliotamalaki kutokana na uchomaji mkaa unaochagizwa na miti kukatwa kiholela ili kusafisha ardhi kwa shughuli za kilimo.

Kikao cha kijiji cha Lengusero,03/06/2021

“Kwanza niwashukuru sana kwa kuweza kutembelea kijiji chetu cha Lengusero ambacho kina changamoto ya wafugaji wanaolalamikia maeneo yao ya malisho yanavamiwa na wakulima”,amesema mkuu huyo wa wilaya na kuahidi kushirikiana na maafisa wa ardhi wilayani humo na hasa kijiji cha Lengusero ili kubaini eneo lililovamiwa.

“Tutakwenda ili tujilidhishe ni namna gani hao wakulima wanapata hayo maeneo yaliyokuwa yanatumiwa kwa ajili ya malisho na kubaini wahusika wote wanaowapa wakulima maeneo ya wafugaji,ameongeza mkuu huyo wa wilaya.

Mnamo June 2,kijiji cha Lengusero ,kilifanya kikao cha kijiji kujadili msitakabali wa mgogoro huo unaofukuta chini chini,ambapo miongoni mwa waliohudhuria walikuwa George Kifuku (Mwenyekiti wa Usuluhishi wa migogoro ya malisho na wakulima) pamoja na Thomas Nkola (katibu),wote kutoka chama cha wafugaji Tanzania.

Viongozi kutoka Chama cha wa Wafugaji wakiwa katika kikao-Lengusero

Katika kikao hicho kilichokaa kwa zaidi ya saa sita,wakazi wa eneo hilo pamoja na mambo mengine walieleza kuwa uvamizi wa maeneo ya malisho pia umeathiri elimu kwa watoto wao.

“Mashamba mengi yanalimwa,na yalikuwa na wanyama pori wasumbufu kama Tembo ambao siku hizi wamehamia jirani na makazi,wanatanda njiani asubuhi na kufanya watoto wetu waogope kwenda shule”,Josepha Palingo aliwaeleza viongozi wa chama wafugaji katika mkutano wa kijiji walioahidi kulifikisha suala hilo pamoja na mengine yote katika mamlaka za serikali.

Baadhi ya wanawake waliohudhuria kikao.

Shule pekee ya msingi  Mbogoi Lengusero iliyopo katika kijiji cha Lengusero imeandikisha wanafunzi 500 wanaotoka pia vijiji vya jirani.Kwa mujibu wa moja ya walimu katika shule hiyo aliyezungumza na muandaaji wa ripoti hii,ni wanafunzi 300 tu au chini zaidi wanahudhuria masomo kila siku na wengine wakishindwa kwa tishio la kushambuliwa na wanyama aina ya Tembo wakiwa njiani kueleke shule na hasa wanaotoka vijiji jirani.

Idadi ndogo ya wanafunzi-S/M Mbogoi Lengusero

Kijiji cha Lengusero kilianzishwa mwaka 1995,kikikaliwa zaidi na watu wa kabila la Maasai linalodai tangu kuanzishwa kwa kijiji, shughuli yao kuu ni ufugaji lakini sasa wanakosa malisho baada ya wageni wanaodaiwa kuletwa na diwani wa kata ya Mkindi na kupatiwa maeneo makubwa kwa ajili ya kilimo kutokana ardhi yao kuwa udongo wenye rutuba.