February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

DAR:VIJANA WATANO HAWAJULIKANI WALIPO TANGU BOXING DAY

Picha:Vijana Watano wanaodaiwa kupotea.

Na Leonard Mapuli (lennymapuli@gmail.com)

Watu watano (Vijana wa Kiume)ambao ni wafanyabiashara katika eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam hawajulikani walipo,baada ya kutoonekana tangu Desemba 26 (Boxing day) mwaka jana.Watano hao,wanaaminika kuwa walienda kujivinjari katika ufukwe wa bahari,eneo la Kigamboni,lakini tangu siku hiyo walipoenda,hawajaonekana tena.

Kwa mujibu wa moja ya ndugu wa waliopotea (Jina tunalo),mawasiliano ya mwisho ya mmoja wa vijana hao,alidai kuwa walikamatwa na askari polisi,lakini taarifa hiyo haikuweka bayana kuwa ni polisi wa kituo gani,na hivyo kuleta ugumu kwa ndugu kujua waende kituo kipi cha polisi kufuatilia.

Hali hii ya sintofahamu,iligeuka kibarua kwa ndugu wa vijana hao,kutembea katika vituo mbalimbali vya polisi na Hospitali jijini dar es Salaam,katika harakati za kuwasaka ndugu zao ili kuwapata wakiwa hai au vinginevyo,juhudi ambazo hazijazaa matunda hadi sasa.

Ndugu mmoja wa kijana aliyepotea,amedai kufika katika baadhi ya vituo vya polisi na kuwaeleza kuhusu tukio hilo,lakini polisi wamekuwa wakijibu kuwa wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

Kamanda wa polisi Kanda maalumu ya Dar es Salaam,Muliro Jumanne,amekiri kupokea taarifa za kutopotea kwa vijana hao,na kwamba Jeshi la Polisi katika eneo lake la kazi,linaendelea na uchunguzi.Kamanda Muliro amewaambia ndugu wa vijana hao wasiojulikana waliko kuwa “si kila aliyepotea yupo mikononi mwa Polisi,na si ikila aliyepotea atakuwa ameuawa’’ na kwataka wawe watulivu wakati uchunguzi unafanyika.

Kwa mujibu wa Tabu Said,mama wa mmoja wa waliopotea,anasema kaka yake (Aliyepotea) aliomba gari mnamo Desemba 26,akidai kuwa walipanga kwenda ufukweni Kigamboni yeye na Rafiki zake,na alifika nyumbani majira ya mchana na kisha kuchukua gari.Mama huyo amezidi kueleza kuwa,baada ya kuchukua gari na kuondoka,hakumtafuta tena hadi ilipofika usiku sana ndipo akaamua kumpigia simu mwanae ambapo simu haikuwa hewani.Hakuwa na wasiwasi kwani aliamini kuwa mwanae huyo pengine angeweza kurudi tu,lakini kukakucha bila kijana huyo kuwa amerudi nyumbani,na ndipo wasiwasi ukamjaa,na alipojaribu tena kupiga simu,bado haikuwa inapatikana.

Taarifa za awali kutoka kwa ndugu,jamaa,na marafaiki wa vijana hao,zinadai kuwa mawasiliano ya mwisho baina yao kabla ya kupotea,walidai kukamatwa na Polisi wakati wakielekea ufukweni (Beach).

Hata hivyo,moja ya ndugu wa vijana hao,amesema kwa hatua ilipofikia sasa,wanamuomba waziri wa mambo ya ndani ya nchi,Hamad Masauni,kuingilia kati sakata hilo,ili kubaini ni wapi vijana hao walipo,wako hai,ama vinginevyo.