February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

CHRAGG YABAINI UTESAJI WA POLISI KWA WATUHUMIWA, YATAKA TUME HURU KUWACHUNGUZA

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imebaini vitendo vya kupigwa na kuteswa kwa watuhumiwa wakati wa ukamataji, au wakati upelelezi ukiendelea kwa madhumuni ya Jeshi la Polisi kupata taarifa zinazohusu matukio ya uhalifuhali inayopelekea watuhumiwa kupata madhara ya mwili na wakati mwingine kupoteza maisha.
 
Katika Tamko lililotolewa hapo jana na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu kuhusu Tathmini ya THBUB kuhusu mwenendo wa Jeshi la Polisi nchini amesema mbali na kupigwa kwa watuhumiwa pia wamebaini kuwepo kwa tuhuma za rushwa dhidi ya baadhi ya askari.
 
“Baadhi ya Askari Polisi kutoa taarifa zisizo sahihi kuhusu vitendo
wanavyolalamikiwa na wananchi na Askari Polisi wanaopatikana na hatia kupewa adhabu isiyowiana na kosa husika,” amesema Jaji Mstaafu Mwaimu.
 
Aidha ameongeza kuwa baadhi ya watuhumiwa wanaokamatwa na polisi wamekuwa wakiwekwa mahabusu za polisi kwa muda mrefu bila ya kupelekwa mahakamani ama kupewa dhamana kinyume na sheria.
 
Pia Jaji Mstaafu Mwaimu ametaka Tume huru za umma au chombo kitakachoundwa kisheria kuchunguza Makosa yanayofanywa na askari polisi yenye mwelekeo wa kijinai.
 
“Kwa kwa lengo la kuleta ufanisi na kuepuka vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora, Jeshi la Polisi lihakikishe utendaji wao wa kazi unazingatia Sheria, Kanuni na miongozo ya utekelezaji wa majukumu ya Jeshi hilo” amesema
 
Kwa upande mwingine Tume ya Haki za Bindamu na Utawala Bora imetoa wito kwa jamii kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili kusaidia kuzuia na kupambana na vitendo vya uhalifu nchini.