March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

CHANJO MPYA YA MALARIA NI TUMAINI JIPYA KWA AFRIKA?

Na Leonard Mapuli


Shirika la Afya Dunia WHO limeidhinisha kwa mara ya kwanza chanjo dhidi ya ugonjwa hatari wa Malaria.
Chanjo hiyo itakayotolewa mara nne kwa kila mtumiaji,inatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa, vifo vya watoto hasa katika nchi za Afrika,kusini mwa Jangwa la Sahara.


Kwa mujibu wa taarifa ya WHO,chanjo ya kwanza itakuwa ikitolewa kwa watoto wanapofikia miezi Mitano,huku chanjo ya pili ikitolewa tena kwa watoto watakapotimiza miezi 6.Chanjo ya Tatu itatolewa kwa walio na umri wa miezi 7,na ya mwisho itatolewa kwa watoto watakapotimiza miezi 18.


Majaribio ya chanjo hii yalianza tangu mwaka 1980 nchini Ubelgiji ambapo takribani miaka 40,wataalamu wamekuwa wakiendelea na tafiti mbalimbali juu ya ufanyaji kazi wa chanjo hii ili kunusuru maisha ya watoto barani Afrika ambako madhara yamekuwa ni makubwa mno.


Kabla ya kuidhinishwa,chanjo hiyo hiyo imefanyiwa majaribio ya mwisho mwaka 2019 katika nchi tatu za Afrika mbazo ni Kenya,Malawi,na Ghana na imeonesha mafanikio makubwa baada ya kutolewa kwa watoto 800,000 wanaoishi katika nchi hizo.


Hata hivyo,ufanisi wa chanjo hiyo si wa asilimia 100 kutokana na kimelea cha plasmodium kinachosababisha Malaria,kuwa na uwezo mkubwa wa kukwepa mfumo wa kinga ya mwili (Immunity) na hivyo kusababisha madhara makubwa ikiwemo vifo.


“Malaria imeziteka nchi za kusini mwa jangwa la Sahara kwa karne nyingi sasa,imesababisha madhara makubwa baada ya kuwakumba watu wengi”,amesema Dkt. Matshidiso Moeti,Mkurugenzi wa WHO,Ukanda wa Afrika.


Shirika la Afya duniani WHO,limependekezo chanjo hiyo aina ya RTS,S/AS01 ielekezwe zaidi katika nchi zilizoathiriwa zaidi na ugonjwa huo kwa mujibu wa tafiti mbalimbali ziliwahi kufanywa na shirika hilo.


“Tukiitumia chanjo hii kama nyenzo muhimu na ya juu kabisa ya mapambano dhidi ya Malaria,tutakwenda kuokoa maisha ya watoto makumi kwa maelfu kila mwaka”,amesisitiza Dr Tedros Adhanom Ghebreyesus,Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Dunia,WHO.


Ugonjwa wa Malaria umetajwa kuua idadi kubwa ya watu barani Afrika,wengi wao wakiwa wanawake wajazito na watoto,ambapo kwa mujibu wa WHO,watoto zaidi ya 260,000 hufariki kwa Malaria kila mwaka barani Afrika.