Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kiko tayari kuzungumza na vyama vya siasa vya upinzani, kuhusu masuala yanayohusu demokrasia na maridhiano.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, katika kongamano la haki, amani na maridhiano, lililoandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), na kufunguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
“Nataka niwahakikishieni, CCM itakuwa tayari kukutana na vyama vyote ili kujadiliana masuala yanayohusu maridhiano, amani pamoja na demokrasia,” amesema Kinana.
Kinana amevitaka vyama vya siasa vya upinzani, kutosusia vikao vinavyoitishwa kwa ajili ya kujadili changamoto zao.
“Nivisihi vyama, nianze na mimi mwenyewe, tunapoitana tukutane hata kama tuna tofauti zetu hatukubaliani kwenye mambo mengi , tukikutana polepole yale tusiyokubaliana yatapungua na hatimaye tukayapunguza kabisa,” amesema Kinana.
Kinana amewahakikishia mabalozi waliohudhuria kongamano hilo kuwa, Serikali itajitahidi kuimarisha umoja wa kitaifa.
“Nashukuru mabalozi kwa heshima mliyotupa, nina hakika mnaipenda nchi hii, mnapenda kuona maendeleo ya nchi hii. Maendeleo ya nchi yanaanza na umoja wa kitaifa na sisi tungependa kufika hatua hii,” amesema Kinana.
Kinana ametoa kauli hiyo ikiwa imebaki siku moja, akabidhiwe uenyekiti wa TCD, kutoka kwa Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.
Kinana ameahidi atakapokabidhiwa uenyekiti wa TCD , ataimarisha mshikamano wa vyama vya siasa.
“Kama mwenyekiti ninayekuja, nitajitahidi kuvikutanisha vyama ili tuweze kuwa na mshikamano, tuelewane vizuri zaidi tuweze kuijenga nchi yetu,” amesema Kinana.
Habari Zaidi
DCI KINGAI ASISITIZA WAZAZI KUZINGATIA MALEZI BORA KWA WATOTO WAO ILI KUPUNGUZA UKATILI
THRDC,C-SEMA YAENDESHA MAFUNZO KWA POLISI NA WAENDESHA MASHITAKA