February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

CCM YAAGIZA MWENENDO WA JESHI LA POLISI UANGALIWE UPYA

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya  Taifa (NEC), ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imempongeza Rais Samia kwa kuunda tume ya uchunguzi wa matukio ya mauaji, huku ikiagiza mwenendo wa Jeshi la Polisi uangaliwe upya.

Akitoa maazimio ya kamati hiyo, jana Jumamosi, jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka, alisema mwenendo wa Jeshi la Polisi nchini hauridhishi kutokana na baadhi ya maofisa na askari wake, kwenda kinyume na miongozo yao ya kazi.

“Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, imempongeza Rais Samia kwa uamuzi wake wa kuunda tume ya kufuatilia matukio mbalimbali ya uhalifu na kupelekea baadhi ya Watanzania kuuawa katika Mkoa wa Mtwara na Tanga,”alisema Shaka na kuongeza:

“Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, imeielekeza Serikali kuangalia upya mwenendo wa Jeshi la Polisi nchini, ambao umekuwa hauridhishi na kulalamikiwa na wananchi kutokana na matendo yanayofanywa na baadhi ya maofisa na askari wa jeshi hilo, kinyume na muongozo wa utendaji kazi wa Jeshi la Polisi.”