February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

CAG AWEKA WAZI CHANGAMOTO ZA MAGEREZA NCHINI, ABAINI UCHAKAVU WA MAJENGO WANAYOLALA WAFUNGWA

Na: Anthony Rwekaza

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amesema kati ya ukaguzi uliofanyika ni pamoja na kuhakiki majengo ya makazi ya magereza, ambapo ameeleza kuwa walibaini majengo mengi ni chakavu na yanahitaji kufanyiwa ukarabati mkubwa.

CAG huyo ameeleza kuwa kulingana na ripoti hiyo iliyokabidhiwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan kama sheria na taratibu zinavyoelekeza, kuwa wamebaini kuwa hali ni mbaya katika yashughulika na kilimo, ambapo amebainisha kuwa wafungwa wamekuwa wakilala kwenye vyumba vilivyojengwa kwa miundombinu hisiyostaili, amesema kuwa hali hiyo hiyo imebainika kwenye Gereza la Ushora na Kingurungundwa.

“Hali mbaya zaidi ilibainika katika magereza ya kilimo ambapo wafungwa walikuwa wakilala katika vyumba zilivyojengwa kwa mabati. Hali hii ilibainika katika Magereza ya Kilimo ya Ushora na Kingurungundwa,” Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)

Pia ameeleza kuwa bweni la wafungwa wanaoshughulika na kilimo la Ushora lilipigwa picha na kuonekana likiwa limezungushiwa mabati yaliyoonekana kuchoka.

Ameongeza kuwa hata nyumba nyingi za watumishi wa Magereza zilizotembelewa katika ukaguzi zilikuwa katika hali mbaya kutokana na kukosa matengezo na ukarabati, ambapo amedai kuwa nyumba nyingi hazikuwa na maji safi na yakutosha.

“Nyumba nyingi za wafanyakazi wa magereza zilizotembelewa zilikuwa katika hali mbaya kwa sababu ya ukosefu wa matengenezo na ukarabati. Nyumba za watumishi wa magereza zilikosa maji safi na ya kutosha.” Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)

Aidha ameeleza kuwa mifumo ya majitaka ilikuwa chakavu na mingi ilikuwa ikivuja. Ambapo amedai kuwa hali hiyo ilibainika katika magereza sita ambayo ni magereza makuu ya Keko na Butimba, Magereza ya Wilaya za Kilwa, Manyoni, na Ukerewe, na Magereza ya kilimo ya Kingurungundwa na Kwa Mngumi.

Amebainisha kuwa licha ya changamoto hizo Jeshi la Magereza halikuwa na mipango ya kufanya matengezo ili kusaidia shughuli za ukarabati wa majengo, lakini ameongeza kuwa kuhusu hali hiyo kwamba hakuna bajeti yoyote iliyotengwa kwa ajili ya kuelekezwa kwenye jukumu la matengenezo na ukarabati.

“Jeshi la Magereza halikuwa na mipango ya matengenezo ili kusaidia shughuli zake za ukarabati wa majengo na hakukuwa na bajeti iliyotengwa kwa madhumuni ya ukarabati na matengenezo.” ameeleza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),

Amesema kuwa kutokana na ukarabati na matengenezo hayo ya miundombinu ya magereza kukosa bajeti, ni kuwa shughuli hizo ziliachwa kwa magereza husika, ambapo ameeleza kuwa jukumu la ukarabati lilifanyika kwa kutumia vyanzo vya fedha vya ndani ya magereza husika.

Vilevile ameeleza kuwa kutokana na ufinyu wa fedha, ukaguzi walioufanya ulibaini kuwa kwa magereza yote 15 yaliyotembelewa, walibaini kiasi cha shilingi milioni 38 kilipelekwa kwa magereza husika kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za askari isipokuwa Wilaya ya Ukerewe iliyopokea shilingi milioni 76 kutokana na hali ya nyumba za maofisa wa magereza kuwa mbaya zaidi.

Amesema kuwa fedha hizo zilizotolewa zilitoka kwenye vyanzo mbalimbali hususani kutoka kwenye miradi ya uwekezaji ambayo inatekelezwa na Jeshi la Magereza katika maeneo mbalimbali Nchini.

“Imeelezwa kuwa, fedha zilizotolewa zilitoka katika vyanzo mbalimbali kama vile faida iliyotokana na miradi ya uwekezaji inayotekelezwa na Jeshi la Magereza nchi nzima.”Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),

Itakumbukuwa baadhi ya wanasiasa, wanaharakati pamoja na taasisi mbalimbali zinazotetea haki za binadamu kwa mara tofauti wamekuwa wakieleza changamoto zinazowakabili wafungwa na watuhumiwa walioko kwenye Magereza mbalimbali Nchini ambapo udai kuwa changamoto hizo zinaweza kuwa kikwazo cha kukosa haki za msingi.

Ripoti hiyo ya mwaka 2021 imegusa maeneo mbalimbali, ikiwemo mikataba mbalimbali iliyofanyiwa na Serikali, taasisi za Umma na binafsi, idara mbalimbali pamoja na maeneo mengine, ikiwa pia imetoa mapendekezo kwenye maeneo yaliyoonekana kuwa na changamoto.