February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

BUNGE LAMPA TANO RAIS SAMIA UZINDUZI WA ROYAL TOUR MAREKANI

IKIWA imepita siku moja tangu Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kuzindua makala maalumu ya kutangaza vivutio vya utalii nchini, Bunge limempongeza kwa hatua hiyo.

Pongezi hizo za Bunge zimetolewa leo Jumanne, jijini Dodoma na Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, kwa niaba ya wabunge.

Spika Tulia ametajasa sababu za Bunge kumpongeza Rais Samia, akisema amejibu kilio cha wabunge juu ya uwepo wa mikakati ya kuongeza idadi ya watalii Tanzania.

“Tunatambua siku ya jana Rais Samia Suluhu Hassan, amezindua makala maalumu ya kuhamasisha utalii Tanzania na kwa sababu wabunge huwa mnachangia kuhusu kuongeza idadi ya watalii wanaokuja, sisi kama Bunge tunampongeza Rais kwa hatua anazochukua kwenye hili eneo,” amesema Spika Tulia.

Licha ya Pongezi hizo, Spika Tulia amewataka wabunge wafuatilie mikakati ya Rais Samia katika kutangaza utalii, ili washauri mahali ambako kutakuwa na mapungufu.

“Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii itakuja baadae, ni muhimu kila mbunge afuatilie mambo yanayoendelea huko ili kama kutakuwa na la kushauri hapa na pale, itakuwa rahisi zaidi. Baada ya kujua hatua mbalimbali zitakazochukuliwa na zile mnazotamani ziongezeke,” amesema Spika Tulia na kuongeza:

:Baada ya hapo ni muhimu kufuatilia ziara hii ya Rais Marekani ya kutangaza Taifa letu Tanzania.”