March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

BULAYA AHOFIA MUSTAKABALI WA WANAHABARI SAMIA AKIONDOKA MADARAKANI

 Mbunge wa Viti maalumu, Ester Bulaya, amehofia juu ya mustakabali wa waandishi wa habari endapo Rais Samia Suluhu Hassan, ataondoka madarakani bila ya kurekebisha baadhi ya vifungu vya sheria ya habari kandamizi.
Bulaya ameonesha wasiwasi huo leo Ijumaa, akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kwa mwaka wa fedha wa 2022/23, bungeni jijini Dodoma.
Mbunge huyo viti maalumu amesema, kwa sasa waandishi wa habari wamepata ahueni kutokana na Rais Samia kuwa na dhamira njema juu yao, na kwamba endapo akiondoka akija kiongozi asiye na dhamira njema, huenda wakakumbana tena na vitendo vya unyanyasaji ikiwemo kutekwa na wasiojulikana pamoja na kukamatwa.
Bulaya ameshauri sheria za habari zirekebishwe ili kulinda maslahai ya wanahabari pamoja na kuimarisha uhuru wa kujieleza na ukosoaji wenye lengo la kuijenga nchi.
“Lakini kwa dhamira tu, leo anaweza mama Samia akamaliza muda wake na ana dhamira njema. Lakini wakaja wengine ambao hawana dhamira njema bado tukarudi kulekule kwa waandishi kupigwa, kuteswa, kunyimwa habari kwa maslahi ya Watanzania,” amesema Bulaya.
Sambamba na hayo, Bulaya amesema nchi inahitaji kurejea katika zama ambazo kuliwa na uhuru kwa waandishi wa habari na wachambuzi, katika kuchambua masuala mbalimbali yenye tija kwa taifa.
“Mbali ya kwamba kuna unafuu lakini bado kuna maeneo mengine waandishi wanatishwa, bado waandishi hawafanyi kazi wka uhuru. Leo hakuna habari za uchunguzi hatahizi makala zinazoandikwa ni za kawaida,” amesema Bulaya na kuongeza:
“Sheria hii ikiletwa kutakuwa na mijadala ya kujenga na kukosoa taifa letu lakini ya kujenga. Tunataka turudi enzi hizo. Tunataka tuone makala za uchunguzi na wachambuzi watakuwa huru kwa maslahi ya taifa.”