February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

BAADA YA UJAMBAZI:UTEKAJI WAREJEA DAR,WAWILI WATEKWA MCHANA KWEUPE.

Aboubakari Fumbo-M/Kiti UKUKAMTA aliyetekwa.

Hofu kubwa imetawala wakazi wa Buguruni Rosana jijini Dar es Salaam kufuatia kutekwa kwa watu wawili mchana kweupe (Saa 6 mchana) siku ya jana (mei 27).Waliotekwa ni ndugu Aboubakari Fambo  mkazi wa Vingunguti ambae ni mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya mkutano wa uzinduzi wa Umoja wa Kudai katiba Mpya Tanzania (UKUKAMTA).

Taarifa za awali zinadai kuwa wawili hao walikuwa wakiratibu uzinduzi wa umoja huo uliopangwa kufanyika eneo hilo la Buguruni siku ya Jumamosi,Mei 29.

Kwa mujibu wa shuhuda wa tukio hilo (Jina tunalo),magari mawili,moja aina ya Toyota Harrier, na jingine aina ya Toyota Noah,yaliegeshwa kando na walipokuwa wamekaa wawili hao,na watu watano walishuka katika magari hayo na kuwakamata kwa nguvu kisha kuwaingiza kwenye moja ya magari yale na kuondoka nao.

“Waliwapakia na wakaondoka nao kuelekea kituo cha Polisi lakini magari hayo hayakupita polisi,yalipitiliza”,amesema shuhuda huyo.

Watetezi Tv imejaribu kufuatilia tukio hili,lakini kwa mujibu wa Polisi kituo cha Buguruni,watu hao hawapo kituoni hapo wala taarifa zao, huku baadhi ya ndugu wa waliotekwa  wakidai kuwa kuna uwezekano wa Aboubakari na Said kuwa wapo kituoni hapo kwa siri.

“Tunahisi walipitiliza kituoni na baadae wakarudishwa kwa usafiri mwingine,ngoja tusubiri tuone”,amesema mwanachama mmoja wa umoja huo.

Mke wa mwenyekiti wa  Umoja wa Kudai katiba Mpya Tanzania (UKUKAMTA) Bi.Mwajuma Venance Mrope ni miongoni mwa watu ambao mpaka sasa wanahangaika  huku na kule ikiwemo polisi kutafuta taarifa kuhusu wapi alipo mumewe na wenzake.

Baadhi ya wanachama wa UKUKAMTA wanahusisha kukamatwa kwa wenzao na uzinduzi wa chama chao,na hofu imewatawala wakihofia pia kukamatwa huku wakisema uzinduzi uko pale pale.

“Wao hata kama wamemkamata mwenyekiti,sisi uzinduzi wetu upo pale pale,siku ya Jumamosi saa nne asubuhi”,amesisitiza mwanachama mmoja wa UKUKAMTA.

Leo ni siku ya pili tangu kutekwa kwa watu hao bila taarifa rasmi ya Polisi ambao wapo kwenye mkakati wa kupunguza uhalifu jijini Dar es Salaam.