February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

BAADA YA OPARESHENI DAR,SIRRO ATANGAZA KIAMA NCHI NZIMA

IGP Sirro alipokutana na kikosi kazi June 9.

Na Leonard Mapuli.

Jeshi la polisi kanda maalumu ya Dar es Salaam limetangaza kumaliza oparesheni  ya kubaini wahalifu wa makosa mbalimbali katika jiji la Dar es Salaam ambapo limesema imekuwa ya mafanikio makubwa na kwamba wahalifu wengi pamoja na silaha zimekamatwa katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.

“Tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa sana,silaha ningi zimekamatwa na wahalifu wengi wamekamatwa”,amesema mkuu wa polisi nchini IGP Simon Sirro bila kutaja idadi, alipozungumza na wandishi wa habari kuhusu kumalizika kwa oparesheni hiyo.

Jeshi hilo lililazimika kuanzisha oparesheni maalumu jijini Dar es Salaam mara baada ya kuibuka kwa matukio mfululizo ya uhalifu wa kutumia silaha uliojitokeza katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam na kusababisha mauaji ya mtu mmoja aliyeuawa kwa kupigwa risasi na walioshukiwa kuwa majambazi.

IGP Sirro amesema kufanikiwa kwa oparesheni hiyo kumechangiwa na ushirika wa viongozi mbalimbali kuanzia wenyeviti wa serikali za mataa na watendaji wa kata zote za jiji la Dar es Salaam.

“Leo tumehitimisha oparesheni katika jiji la Dar es Salaam na kesho (Juni 9) tunaanza oparesheni ya mwezi mzima nchi nzima”,ametangaza IGP Sirro na kuongeza kuwa oparesheni aliyoitangaza leo kwa nchi nzima itahusisha pia usalama barabarani ambapo magari mabovu yote yatakamatwa na madereva wazembe watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.

Wakati huo huo jeshi hilo limeonya vikali watu wote wanaojihusha na uhalifu wa aina yoyote kuacha mara moja kwani halitamvumilia mhalifu yeyote atakaejaribu na kubainika kufanya uhalifu.

“Wale wahalifu wanaotoka na kufanya uhalifu Mbaya Mbaya wasilalamike na sisi tukiwfanyia mambo Mabaya Mabaya”,amesema IGP Siro wakati wa kikao kazi cha kufanya tathmini, mafanikio na changamoto katika kubaini mianya ya uhalifu na wahalifu.