February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

BAADA YA OLENGURUMWA NA WADAU KUISHAURI SERIKALI ,NCHEMBA ASEMA RAIS AMESIKIA

Siku moja baada ya Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa haki za binadamu Tanzania (THRDC), Wakili Onesmo Olengurumwa pamoja na wadau wengine kuihasa Serikali kufanyia marekebisho tozo mpya kwenye miamala ya simu,rai hizo zimemuibua Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba.

Waziri Nchemba ameuelezea umma wa Tanzania kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameguswa kilio cha wananchi na tayari ameshawaagiza kuwa jambo hilo lifanyiwe kazi kwa kina ili kuondoa malalamiko.

“Mhe. Rais naye ameguswa na jambo hili, amesikia maoni ya Watanzania wote, ameshatoa maelekezo kwamba tuyafanyie kazi haya malalamiko ambayo wananchi wanayatoa.” – Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba.

Waziri Mwigulu ametoa rai kwa wananchi kuwa kufuatia maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan tayari Waziri Mkuu ameshaitisha kikao maalumu kitakachofanyika kesho jumanne, Julai 20,2021 ili kujadili masuala hayo ya tozo mpya.

“Nitoe rai kwa wananchi kuwa Serikali imesikia malalamiko ya wananchi na tayari tunaendelea kuyafanyia kazi, Waziri Mkuu ameshaitisha kikao kesho kuendelea kupitia masuala haya haya.” amesema Waziri wa Fedha na Mipango Mwigulu Nchemba.

Pia Waziri Mwigulu amesema kuwa kutokana na Sheria hiyo tayari kupitishwa na Bunge hivyo inatakiwa kutekelezwa licha ya uwezekano kufanyiwa marekebisho kwa kwenye kanuni zinazoangukia kwenye Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Teknolojia ya Mawasilino.

“Kwa sababu hii ni sheria ya Bunge, na tayari imeshapitishwa na inatakiwa kutekelezwa, lakini kuna maeneo ambayo yanaangukia kwenye kanuni ambazo zinaangukia Wizara ya Fedha na Wizara ya Teknolojia ya Mawasiliano.” amesema Waziri Fedha na Mipago, Mwigulu Nchemba

Ikumbukwe jana kwenye kipindi Mizani ya Wiki kinachorusha na kituo cha runinga cha Azam TV, Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa haki za binadamu Tanzania (THRDC), Wakili Onesmo Olengurumwa alitoa mapendekezo kwa Serikali ikiwa ni kutathimini kiwango cha tozo kwenye baadhi ya miamala ambacho hakitakuwa kero na kilio kwa wananchi, hususani maskini.

Zikiwa zimepita siku nne baada ya Serikali kuanza kutekeleza Sheria hiyo ya tozo kwenye miamala ya simu iliyopitishwa na Bunge kwenye bajeti ya mwaka mpya wa fedha 2021/2022, ambayo tayari imeanza kutekelezwa July mosi wadau mbalimbali pamoja na wananchi kwenye maeneo tofauti wameibuka na kutoa maoni yao kuhusu tozo hizo.