February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

AUWAWA KISA UZURURAJI

Hatimaye Mwili wa Kijana Denis Petro (20) aliyedaiwa kuuwawa na Mwenyekiti wa mtaa wa Nyambiti anayejulikana kwa jina la Itale Zeba, umepumzishwa leo kwenye nyumba yake ya milele baada ya kuwepo na mvutano baina ya wananchi na polisi  hasa baada ya wanakijiji kufukia kaburi alilotakiwa kuzikwa kijana Denis huku wakishinikiza mamlaka husika kufanya uchunguzi ili haki ipatikane.

Baada ya vuta nikuvute ya muda hatimaye jeshi la polisi lilifanikiwa kutuliza ghasia na kuamuru kufukuliwa kwa kaburi hilo ili mwili wa kijana Denis uzikwe huku jeshi hilo likiwataka wananchi kuwa watulivu na kulipa nafasi ya kufanya kazi yake.

Duru zinadai kuwa marehemu Denis alikamatwa na mwenyekiti huyo siku ya tarehe 14 mwezi huu, na kupigwa kwa madai ya kuzurura bila sababu hadi alipofikwa na umauti.

Mama mzazi wa Denis anayefahamika kwa jina la Lucia Mulamula amezungumza na Watetezi TV huku akielekeza kilio chake kwa mamlaka husika na kuziomba kumwezesha kupata haki yake ya kuchunguzwa kwa tukio la kifo cha mwanaye Denis.

Naomba sheria inipiganie, mimi ni mama mjane huyo aliyeondoka ndio alikuwa akitoka kwenda hata kutafuta sabuni. Laiti kungekuwa karibu, ningeweza kwenda hata kwa Rais Samia nimlilie Miguuni. Hili swala la kukandamizwa, naona hata viongozi wengine wanakandamiza kwa kuwa wananiona mimi ni mwanamke sina uwezo wowote wa kufuatilia chochote vijana wananyanyasika wanapigwa bila makosa

Lucia MulaMula mama mzazi wa Denis

Tunaomba serikali kuu itusaidie sisi vijana, ambao kesho na keshokutwa tusije kuumia, kwani mpaka sasa wanaandika majina ya vijana ambao wanasema ni viherehere na mpaka sasa hivi tunatishiwa, wanatuambia tutaona kwani hili si tukio la kwanza ni tukio la nne

Mwananchi

Wananchi wa kata hiyo wameiomba serikali kuliangalia kwa undani swala hilo kwani tukio hilo linadaiwa kuwa si tukio la kwanza katika kata hiyo ya Buzuruga.