February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

“APP” YA KWANZA YA KUSAIDIA WANAWAKE KISHERIA YAZINDULIWA TANZANIA.

Na Leonard Mapuli.

Shirika lisilokuwa la kiserikali la Legal Services Facility (LSF) linalofanya shughuli za utoaji misaada ya kisheria hasa kwa wanawake nchini Tanzania limezindua Mtandao (App) ambayo itatumiwa na watu wote watakaohitaji msaada wowote wa kisheria kupitia shirika hilo.

App hiyo   inayotambulika kama HAKI YANGU itakuwa na uwezo wa kumuunganisha mhitaji wa msaada na mtoa huduma anayetambulika na shirika na itatumika katika mikoa yote ya Tanzania ambapo mhitaji atasaidiwa muda huo huo. Hii imelifanya shirika hilo kuwa la kwanza binafsi kutoa huduma  za msaada kisheria kidigitali zaidi nchini Tanzania.

Akiielezea huduma hiyo kwa vitendo,meneja wa uangalizi na matokeo kutoka shirika hilo Said Chitung amesema App hiyo itaruhusu mawasiliano ya papo kwa papo kati ya mtoa huduma na anayehitaji huduma (Chating) ambapo anayehitaji huduma ataangalia mtoa huduma gani aliyepo mtandaoni (Online) na ataweza kumwandikia ujumbe mfupi kumweleza angehitaji asaidiwe nini kisheria ama anaweza kumpigia simu moja kwa moja kupitia App hiyo.

App ya “Haki Yangu” imebuniwa na kituo hicho ili kuwarahisishia watoa huduma wa msaada wa kisheria kote nchini “Paralegals” kupata elimu na kutoa huduma kwa haraka.

 “Mpaka sasa  Legal Services Facility tunafanya kazi na vituo 4000 vinavyotoa misaada ya kisheria katika mikoa na wilaya zote za Tanzania,na tumefanikiwa kuwafikia watu milioni 6 Tanzania bara na Zanzibar” amesema Lulu Ng’wanakilala, Mkurugenzi Mtendaji wa LFS na kuongeza kuwa kwa kutumia App ya Haki Yangu,watu wengi zaidi watapatiwa msaada wa kisheria.

Wizara ya katiba na sheria imelipongeza shirika hilo kwa ubunifu huo na kuyataka mashirika mengine ya usimamizi na utoaji haki kuja na mbinu nyingi zaidi ili watu wote waweze kupata haki zao bila kuonewa.

“Huduma za LSF zinaangukia moja kwa moja kwenye wizara yangu,hivyo nitaendelea kushirikiana na taasisi zote za serikali na zisizo za serikali kuhakikisha upatikanaji wa haki kwa watanzania na raia wa kigeni” amesema Profesa Palamagamba Kabudi,Waziri wa Katiba na Sheria wa Tanzania aliyekuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa App hiyo

Katika hali ya kushangaza,waziri Kabudi aliuduwaza umma wa waliohudhuria uzinduzi huo pale alipoweka bayana kuwa katika simu yake ya mkononi aina ya Nokia hatumii App yoyote na hivyo kuacha watu midomo wazi.

“Sijawahi kuwa na akaunti Facebook,instagram wala twitter,nikashangaa kuna mtu anatumia majina yangu huko halafu anaandika Kiingereza cha hovyo na mimi Sina Kiingereza cha namna ile”,Prof. Kabudi.

App ya Haki Yangu inapatikana katika mifumo  ya Android na IOS ambapo kila muhitaji atatakiwa kuipakuwa na kuisanikisha katika simu yake ya mkononi ama kibao (Tablet) na kisha kila atapohitaji huduma atawasha data na kuitumia kama zilivyo huduma za kuitisha usafiri za uber,bolt,ama Taxfy katika maeneo mengi duniani.