February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

ALIYEFARIKI KWA KUPIGWA RISASI NA POLISI NA WAWILI KUJERUHIWA, ACT WAZALENDO WATOA TAMKO

Juma Ramadhani Bichuka mkazi wa Mwandiga,mtaa wa Mgera B, inadaiwa ameuwa na askari wa Jeshi la Polisi kwa kupigwa risasi maeneo mbalimbali ya mwili wake katika eneo la uwanja wa Lake Tanganyika Mkoani Kigoma wakati askari hao wakiwa kwenye harakati za kutaka kutuliza vurugu za mashabiki ambao walikuwa wanashudia mchezo wa fainali uwanjani hapo ambapo pia inadaiwa mashabiki wengine wawili nao wamejeruhiwa kwa risasi.

Katika taarifa rasmi iliyotolewa na Chama cha ACT Wazalendo baada ya kuenea kwa madai hayo kwenye mitandao ya kijamii, inasema kuwa Machi 14, 2022 majira ya jioni katika uwanja wa Lake Tanganyika-Kigoma kulikuwa na fainali ya ligi ya Joy (Dr.Livingstone Cup) iliyozikutanisha timu mbili baina Mwandiga FC (Mwandiga Combine) na Kipampa FC ya Ujiji .

Taarifa hiyo imeendelea kueleza kuwa mchezo huo ukiwa unaendelea,mashabiki wa timu hizo mbili waliokuwa katika jukwaa moja, walianza kuzomeana jambo ambalo lilipelekea kuwepo kwa vurugu, na kufuatia vurugu hizo taarifa imedai kuwa Polisi waliingilia na kutumia mabomu ya machozi na mashabiki waliamriwa na MC kuhama jukwaa ili kuwatenganisha jukwaa baina mashabiki wa timu hizo mbili kwa lengo la kuepuka vurugu.

Imeelezwa kwa wakati mashabiki wakiwa wanahama katika majukwaa waliyoelekezwa,Polisi waliokuwepo walipiga risasi mbili juu na risasi mbili zingine akapigwa shabiki moja wa timu ya Mwandiga FC anayeitwa Bw.Juma Ramadhani Bichuka mkazi wa Mwandiga,mtaa wa Mgera B.Risasi moja alipigwa kwenye paja na risasi nyingine alipigwa kwenye tumbo na kupelekea kupoteza maisha.

Pia imeelezwa kuwa licha mtu huyo kupoteza maisha, lakini Polisi risasi nyingine ziliwajeruhi mashabiki wengine wa timu ya Mwandiga FC anayeitwa Omary Amrani (KIRUNGU),mkazi wa Mwandiga, mtaa wa Mgera-A, Shabiki huyo ambaye huyo inadaiwa kwa mujibu wa taarifa kuwa alipigwa risasi ya mguuni na amelazwa kwenye hospital ya maweni.

Shabiki mwingine ambaye amedaiwa kupigwa risasi ni Nasifu Moshi , mkazi wa Mwandiga-Kibingo. Taarifa inaeleza kuwa kuwa shabiki huyo alipigwa risasi kwenye mguu pia yupo hospital ya maweni.

Kufuatia madai hayo ambayo bado Jeshi la Polisi halijatoka kuyatolea ufafanuzi licha ya kusambazwa na kuenea kwenye mitandao ya kijamii, Chama hicho kimetoa mapendekezo kwa Serikali pamoja na Jeshi la Polisi.

Katika mapendekezo yao nane wameshauri kufanyika kwa uchunguzi huru na wa haraka, huku wakipendekeza kusimamishwa na kukamatwa kwa Askari ambao wanatuhumiwa kuhusika ili kupisha hatua za uchunguzi.

” Tunataka uchunguzi huru ufanyike, Kamati huru ya uchunguzi iundwe haraka ili kufanya uchunguzi wa tukio hili huku Polisi ambao wamefanya tukio hili wasimamishwe kazi na wakamatwe ili kupisha
uchunguzi na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. ” Taarifa hiyo imeeleza

Aidha wamependekeza kuwa Serikali na Jeshi la Polisi linapaswa kutoa fidia kwa familia ya marehemu Juma Ramadhani Bichuka,
kwa kuwa alikuwa ana familia na yeye ndiye alikuwa tegemeo katika familia yake kabla ya kuuwawa.
, lakini wapendekeza kuwa Serikali na Polisi wanapaswa kubeba jukumu la matibabu na fidia kwa majeruhi wawili wanaodaiwa kujeruhiwa kwa risasi.

Hata hivyo wamelitaka Jeshi la Polisi kuwaachia huru wananchi wote na mashabiki wa mpira waliokamatwa jana uwanjani wakidai kuwa hawana hatia.

Vilevile katika pendekezo lao la tano wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuangalia namna ya kulifanyia maboresho(kulifumua) Jeshi lote la Polisi
Tanzania kiutendaji, kisheria na kiuwajibikaji, wakieleza kuwa mabadiliko hayo yatalifanya Jeshi hilo kutekeleza majukumu yao vizuri bila kutumia nguvu.

Vilevile ACT Wazalendo wamependekeza kiundwe chombo huru cha kuangazia mienendo ya Polisi “Independent Policing
Oversight Authority” (IPOA), ili kiwe na jukumu la kupokea malalamiko ya wananchi juu ya matendo ya Polisi na kuyafanyia kazi, wamedai kuwa kwa mazingira ya sasa Polisi ikikosea hakuna sehemu ya kupeleka malalamiko.

Aidha wamependekeza iundwe Kamisheni ya maadili ya Jeshi la Polisi, itakayosimamia kusimamia weledi na maadili ya Jeshi la Polisi katika utendaji wao wa kila siku.

Lakini vilevile wamependekeza kuongezwa muda wa Polisi kuhudhuria mafunzo katika vyuo vya Polisi nchini uongezwe ili kuongeza
weledi, taaluma na ufahamu wa majukumu yao katika kutenda haki na kulinda Raia katika jamii. Wameshauri iongezwe kutoka tisa iliyozoeleka na kuongezwa kufikia miaka miwili au mitatu kama zilivyo fani nyingine.