February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

ACT-WAZALENDO YATAKA CHOMBO HURU KULICHUNGUZA JESHI LA POLISI

Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha ACT-Wazalendo, kimeomba chombo huru kianzishwe kwa ajili ya kulichunguza Jeshi la Polisi, kwa ajili ya kubaini baadhi ya watendaji wake wenye utovu wa nidhamu.

Wito huo umetolewa tarehe 7 Machi 2022 na Msemaji wa Kisekta wa Wizara ya Mambo ya Ndani wa ACT-Wazalendo, Mbarala Maharagande, kupitia taarifa yake aliyoitoa kwa umma.

“Kianzishwe chombo huru cha kuchunguza Jeshi la Polisi (Independence Police Oversight body) ili ichunguzwe vitendo vyote vya utovu wa maadili na makosa yanayoweza kuathiri haki za wananchi,” imesema taarifa ya Maharagande.

Wakati huo huo, Maharagande ameshauri zitungwe sheria za kuwawajibisha watendaji wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), watakaokuwa wanakwenda kinyume na maadili ya utendaji wao wa kazi.

“Pawepo na sheria zinazoweka udhibiti wa mamlaka na ofisi ya DPP na watendaji wake, ili pale panapotokea uzembe, nia ovu pawepo na uwajibikaji kisheria. Mamlaka ya DCI na upelelezi wa kesi yaboreshwe na pawepo ukomo wa upelelezi wa kesi za aina hii zisizokuwa na dhamana,” imesema taarifa ya Maharagande.

Maharagande ametoa wito huo baada ya DPP, Sylvester Mwakitalu, kumfutia mashtaka ya ugaidi Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, Hlafan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillha Ling’wenya.

Mashtaka hayo matano ya ugaidi, yalikuwa yanawakili kina Mbowe, katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, jijini Dar es Salaam, kuanzia Septemba 2021.

Akizungumzia hatua hiyo, Maharagande amesema “Mbowe hakushinda kesi, tupiganie kupatikana kwa mifumo imara ya uongozi wa nchi na utoaji haki. Mhimili wa mahakama uwe huru kuendesha masuala yake, siasa isiamue juu ya upatikanaji haki.”