February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

ACT WAZALENDO WATEMA NYONGO WABAINISHA SABABU ZA KUSHIRIKI CHAGUZI ZA MARUDIO

Na: Anthony Rwekaza

Chama cha ACT Wazalendo kimeeleza sababu ya kushiriki kwenye chaguzi za marudio zinazoitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ( NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kwenye majimbo na Kata licha ya kuwepo kwa mbalimbali yanayodaiwa na kuyatafsiri kuwa ni ubinywaji wa Demokrasia Nchini Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Ofisi za chama hicho, zilizopo Kijitonyama Jijini Dar es salaam Jumatatu Oktoba 2021 Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu amesema chama cha ACT Wazalendo kimeshiriki kwenye chaguzi za majimbo yote matano na baadhi ya Kata kufuatia uamuzi utokanao sababu tatu.

Kati ya sababu hizo amesema ni pamoja na kutoa fursa kwa Chama kuyatetea Majimbo na Kata ambazo wamekuwa wakiziongoza kabla ya Mbunge au Diwani ya Chama hicho kufariki, huku akitolea mfano Majimbo ya Pandani na Konde, Kupambana kushinda majimbo na Kata ambazo aziongozwi na Chama hicho na sababu nyingine aliyoibainisha ni kupigania demokrasia kupitia majukwaa ya kampeini.

“Kutoa fursa kwa Chama kuyatetea Majimbo na Kata tunazoziongoza iwapo Mbunge au Diwani wa ACT Wazalendo atafariki au kupoteza sifa za kuendelea kushikilia nafasi yake. mathalani kwenye Majimbo ya Pandani na Konde, Chama kilishiriki kwa ajili ya kutetea nafasi yake kwa sababu Majimbo yalikuwa yanaongozwa na ACT Wazalendo kabla ya chaguzi za marudio kuitishwa, Kupambana kushinda majimbo na Kata ambazo hatuziongozi na kujenga mtandao madhubuti wa Chama, Kupigania Demokrasia kupitia majukwaa ya kampeini” amesema Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu

Pia Ado Shaibu amesema kwenye chaguzi za marudio yapo baadhi ya mambo ikiwemo kwenye michakato ya uteuzi, kampeini na uapishaji wa mawakala, mawasiliano na wadau mamlaka zimejitaidi kuyafanyia kazi, lakini amedai bado zipo changamoto mbalimbali, akitolea mfano Chama Cha Mapinduzi (CCM) kudaiwa kuendelea kula njama na wasimamizi wa Uchaguzi kupita bila kupingwa kwenye chaguzi mbalimbali za marudio, jambo ilo ameliita ‘Kamseleleko’ akiwa na maana kuwa wanapenda uwepesi.

Katibu Mkuu huyo pia amedai Jeshi la Polisi limekuwa likitumia nguvu kubwa kwenye baadhi ya chaguzi mbalimbali kwenye Kata na Majimbo na hili kuthibitisha hilo ametolea mfano tukio la kwenye Kata ya mbagala Kuu kuwa Mgombea wao Shaweji Mketo alikamatwa na kupigwa na kusababishwa majeraha wakati akiwa kwenye harakati za uchaguzi.

“Jeshi la Polisi kutumia nguvu kubwa kwenye baadhi ya Kata ili kutisha wapiga kura na wagombea, mathalani kwenye Kata ya Mbagala Kuu, Mgombea wa ACT Wazalendo Shaweji Mketo alikamatwa na kupigwa na kujeruhiwa mguu na Jeshi la Polisi wakati akitumia haki yake ya kutembelea vituo vya kupiga kura” Katibu Mkuu Mkuu ACT Wazalendo, Ado Shaibu

Kufuatia malalamiko ambayo yamekuwa endelevu Chama hicho kimebainisha kuwa kilimuandikia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuhusu kukutana na vyama vya siasa na kufanya mazungumzo juu ya namna ya kuendesha shughuli za kisiasa Nchini katika mazingira ambayo yataepusha malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa mara kwa mara na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa.

Shaibu amesema Rais Saimia alijibu barua hiyo akidai anatambua umuhimu wa demokrasia ya vyama vya siasa Nchini na ataindeleza katika utawala wake, ikumbukwe pia Rais Saimia siku chache baada ya kuapishwa alitoa kauli ya kutaka kukutana na vyama vya siasa kujadili namna na njia njema ya kuendesha siasa Nchini bila mgongano na kwa kuzingatia sheria zimavyoelekeza.

Amesisitiza kuwa huu ndiyo muda muafaka wa Rais Samia kukutana na vyama vya siasa, huku akimtaka Rais Samia kuruhusu mchakato wa Katiba mpya na Tume huru ya Uchaguzi na kudai kuwa huo ndio itakuwa suluhisho ya changamoto mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Ikumbukwe Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wenyewe walibainisha msimamo wao kwa kutoshiriki uchaguzi wowote wa marudio kwenye Majimbo na Kata kwa madai kuwa hawana imani na Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliyo iliyoratibu mchakato wa uchaguzi Mkuu 2020, huku mara kwa mara wamekuwa wakisisitiza dhamira yao ya kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan kama ilivyo kwa ACT Wazalendo.