February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

ACT-WAZALENDO “SERIKALI IFUATILIE MIENENDO YA VIONGOZI WA UMMA”

Chama Cha ACT Wazalendo kimemtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mohamed Mchengerwa kufuatilia kwa karibu mienendo ya viongozi wa umma na kuhakikisha kuwa wanazingatia misingi ya utawala bora katika kutekeleza majukumu yao.

Rai hiyo imetolewa jana tarehe 26 Desemba 2021 na Katibu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu Ado katika kikao na viongozi na wanachama wa ACT Wazalendo wa Jimbo la Tunduru Kaskazini.

“Nimekwenda Tunduru Kusini na leo nipo Tunduru Kaskazini. Kote nimeelezwa kilio cha Wananchi juu ya Mkuu wa Wilaya Ndugu Julius Mtatiro” alisema Ndugu Ado Shaibu na kuongeza;

“Si sahihi kwa Mkuu wa Wilaya, kwa ubabe, kukata fedha za wakulima wa Korosho kuchangia timu ya mpira bila kushirikisha wanachama wa Vyama vya Ushirika (AMCOS). Sio sawa pia kwa Mkuu wa Wilaya kuingilia uendeshaji wa ushirika na kuwalazimisha wananchi kuuza mazao kwa bei ya chini. Nimeelezwa kuwa kwenye kijiji Cha Tulieni, Kata ya Nakapanya, wananchi walipigwa mabomu kwa sababu ya kutafuta bei nzuri ya mbaazi Wilaya ya jirani. Masuala haya yangeweza kushughulikiwa kwa njia shirikishi, sio kwa mabomu”.

Ado amemtaka Waziri Mchengerwa kufuatilia kwa karibu na kuhakikisha kuwa viongozi wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria na misingi ya utawala bora kwa sababu baadhi ya Wakuu wa Wilaya na watendaji wengine wanatumia sana ubabe na vitisho badala ya kuongozwa na ubunifu, maarifa na ushirikishwaji.

Katibu Mkuu akiambatana na Naibu Katibu Mwenezi Janeth Rithe, Katibu wa Sera na Utafiti Idrisa Kweweta na Naibu Katibu Mwenezi Antony Ishika anaendelea na ziara kwenye Mikoa mbalimbali Nchini na leo atakuwa Jimbo la Nanyumbu Mkoa wa Mtwara.