March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MAHAKAMA YA HAKIMU MKAZI ARUSHA, IMEAHIRISHA KESI YA MAUAJI YA ASKARI POLISI ENEO LA LOLIONDO WILAYANI NGORONGORO KUTOKANA NA UPELELEZI WAKE KUTOKUKAMILIKA.

Katika kesi hiyo ya mauaji namba 11/2022 kati ya washtakiwa 24, yumo Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ngorongoro, Ndirango Laizer pamoja na madiwani 10.

Leo Jumanne, Agosti 30, 2022 mbele ya Hakimu Mkazi, Herieth Mhenga kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa.

Baada ya kesi kutajwa Wakili wa Serikali Upendo Shemkole alidai kuwa upelelezi wake unaendelea na wanaendelea kufuatilia na kusisitiza upelelezi ukamilike kwa haraka na kuomba kupangiwa tarehe nyingine kwa ajili ya kutaja kesi hiyo.

Jopo la utetezi lililokuwa na mawakili sita wakiongozwa na Wakili Ernest, waliomba upelelezi huo ukamilike kwa haraka ili watuhumiwa wapate haki kwa wakati.

Watuhumiwa wengine katika kesi hiyo ni Molongo Paschal, Albert Selembo, Lekayoko Parmwati, Sapati Parmwati, Ingoi Olkedenyi Kanjwel, Sangau Morongeti, Morijoi Parmati, Morongeti Meeki, Kambatai Lulu, Moloimet Yohana na Joel Clemes Lessonu.

Wengine ni Simon Orosikiria, Damian Rago Laiza, Mathew Eliakimu, Luka Kursas, Taleng’o Leshoko, Kijoolu Kakeya, Shengena Killel, Kelvin Shaso Nairoti, Wilson Kiling, James Taki, Simon Saitoti na Joseph Lukumay.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na makosa mawili ambapo kosa la kwanza ni njama ya mauaji ambapo wanadaiwa kupanga njama ya kuua maafisa wa serikali na maafisa polisi watakaoshiriki zoezi la kuweka mipaka pori tengefu la Loliondo.

Kosa la pili ni mauaji ambapo wanadaiwa Juni 10, 2022 eneo la Ololosokwan wilayani Ngorongoro kwa nia ovu walisababisha kifo G 4200 Koplo Garlus Mwita.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Sepetemba 13, 2022 itakapotajwa